Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dola bilioni 2.4 zasakwa kunusuru Sahel ya Kati

Mnamo Februari 2020, mji wa Dori ukanda wa Sahel nchini Burkina Faso lilikuwa linahifadhi takriban wakimbizi wa ndani 15,000.
© UNHCR/Sylvain Cherkaoui
Mnamo Februari 2020, mji wa Dori ukanda wa Sahel nchini Burkina Faso lilikuwa linahifadhi takriban wakimbizi wa ndani 15,000.

Dola bilioni 2.4 zasakwa kunusuru Sahel ya Kati

Msaada wa Kibinadamu

Hii leo huko Copenhagen nchini Denmark kunafanyika mkutano wa ngazi ya mawaziri wenye lengo la kuchangisha fedha kwa ajili ya mataifa matatu yaliyo ukanda wa kati wa Sahel ambayo ni Burkina Faso, Niger na Mali kutokana na janga kubwa la kibinadamu linalokabili wakazi wa maeneo hayo.
 

Takwimu zinaonesha kuwa zaidi ya watu milioni 1.5 katika eneo hilo wamelazimika kukimbia makazi yao kutokana na ghasia, idadi ambayo ni mara 20 zaidi ikilinganishwa na miaka miwili iliyopita.

Kama hiyo haitoshi, ukatili wa kijinsia umeongezeka, mamilioni ya watoto hawako shuleni, huduma za msingi za afya na za kijamii hazipatikani.

Kwa sasa hali ya ukosefu wa chakula ni mara tatu zaidi ikilinganishwa na mwaka mmoja uliopita huku umaskin na mabadiliko ya tabianchi vikitishia mbinu za kawaida za watu kujipatia kipato na hivyo kufanya watu zaidi ya milioni 13 kuhitaji misaada ya kibinadamu.

Zore Yusef wakila chakula na mmoja wa watoto wake.Mzozo wa silaha ulilazimisha familia yake kukimbia mkoa wa kaskazini wa Burkina Faso.
WFP/Marwa Awad
Zore Yusef wakila chakula na mmoja wa watoto wake.Mzozo wa silaha ulilazimisha familia yake kukimbia mkoa wa kaskazini wa Burkina Faso.

Miongoni mwao hao ni watoto milioni 7 walioathiriwa na mapigano sambamba na janga la ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19.

Akifafanua kuhusu janga linalokumba wakazi wa Sahel ya Kati hususan Burkina Faso, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la mpango wa chakula la Umoja wa Mataifa, WFP, David Beasley ambaye hivi karibuni ametembelea eneo la Kaya, nchini humo, amesema, “tunaamini kuna takribani watu 11,000 ambao wako kwenye kiwango cha 5 cha njaa na hatuna uwezo wa kuwafikia. Iwapo tunaweza kuwafikia, tunaweza siyo tu kuokoa maisha yao, bali pia kubadili maisha yao. Iwapo tunaweza kuwaleta hapa, tunaweza kushirikiana nao kupanda mazao n hawatategemea msaada wa nje.”

Akizungumzia mkutano huo wa kuchangia fedha, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres amesema, “Sahel ya Kati liko katika msambaratiko. Tunahitaji kubadili mwelekeo kwa kuwa na msukumo mpya wa maridhiano. Halikadhalika tunahitaji msaada wa kibinadamu. Mashirika ya Umoja wa Mataifa na yale ya kiraia yako kwenye eneo hilo yakiunga mkono jitihada za kitaifa. Kwa ufadhili wa kutosha, tunaweza kuchukua hatua zaidi.”

Katibu Mkuu ameongeza kuwa, “hatua za mashirika hayo zimelinda na kuokoa maisha ya mamilioni ya watu kwa kupatia chakula, huduma za msingi za afya ya mwili na akili, maji safi, huduma za kujisafi, malazi na elimu. Na ndio maana tunaomba dola bilioni 2.4 ili kusaidia miezi iliyobakia ya mwaka 2020 na kuwapatia misaada ya dharura hadi mwaka 2021. Naomba msaada wenu.”

Katibu Mkuu amesema msaada wa muda mrefu utapatikana kupitia maendeleo endelevu, utawala bora na fursa sawa kwa wote, hususan vijana.

Hata hivyo amesema hilo haliwezi kupatikana kwa ghafla, bali “tunaweza kuepusha janga hili lisikue na kuwa baya na hatimaye kugharimu zaidi siku za usoni.”

Guterres amesema lazima kuchukua hatua, na kuchukua hatua hivi sasa.

Sahel ya Kati inahusisha nchi za Burkina Faso, Mali na Niger.