Watoto milioni 10 Sahel ya Kati hatarini, huku ukosefu wa usalama ukitishia janga kusambaa nchi jirani- UNICEF

Sophia Sokoka, mwalimu wa shule ya msingi ya umma ya Tchoutchoubou nchini Benin akimsamia Abasse Dahani, mwanafunzi mkimbizi kutoka Burkina Faso kufanya kazi yake ya shuleni.
© UNICEF/ Newson Hounkpatin
Sophia Sokoka, mwalimu wa shule ya msingi ya umma ya Tchoutchoubou nchini Benin akimsamia Abasse Dahani, mwanafunzi mkimbizi kutoka Burkina Faso kufanya kazi yake ya shuleni.

Watoto milioni 10 Sahel ya Kati hatarini, huku ukosefu wa usalama ukitishia janga kusambaa nchi jirani- UNICEF

Msaada wa Kibinadamu

Watoto milioni 10 nchini Burkina Faso, Mali na Niger wana uhitaji mkubwa wa misaada ya kibinadamu, idadi ambayo ni maradufu ikilinganishwa na mwaka 2020, limesema shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto duniani, UNICEF hii leo, chanzo kikiwa ni mizozo inayoshamiri kila uchao na kwamba Watoto wengine million 4 nchi Jirani wako hatarini Zaidi kwani mapigano kati ya makundi yaliyojihami na majeshi ya serikali yanavuka mipaka.

Tuko Benin na sauti ni ya Abasse, Dahani, mtoto mkimbizi mwenye umri wa miaka 8 kutoka Burkina Faso anasema tulikuja hapa Tanguieta Benin kwa mguu. Tulikimbia nyumbani kwa sababu tulifukuzwa.

Abasse anawakilisha mamilioni ya watoto wanaokimbia makwao ukanda wa Sahel kwani Mkurugenzi wa UNICEF  kanda ya Afrika Magharibi na Kati Marie – Pierre Poirier anasema “watoto wanazidi kukumbwa kwenye mapigano kama waathirika wa mapigano au walengwa kutoka vikundi vilivyojihami ambavyo si vya kiserikali.”

Afisa huyo anatolea mfano Burkina Faso akisema watoto waliothibitishwa kuuawa katika miezi tisa ya mwanzo yam waka 2022 walikuwa mara tatu zaidi kuliko mwaka 2021.

Wengi wa watoto hao walikufa kutokanana majerara ya risasi, vijiji vyao kushambuliwa au kulipuka kwa vilipuzi vya kutengeneza au masalia ya mabomu yatumikayo vitani.

 Bi. Poirier amesema mwaka 2022 ulikuwa wa kikatili Zaidi kwa Watoto Sahel ya Kati na hivyo pande zote kwenye mzozo lazima zikomeshe mashambulizi kwa Watoto, shule zao, vituo vya afya na makazi yao.

Mapigano ni ya kikatili zaidi, vikundi vilivyojihami vinatumia mbinu kali

Wazazi wa Abasse,  Ousséni Dahani na Ramatou Yonli wakiwa nje ya nyumba yao huko Benin. Walikimbia Burkina Faso baada ya kijiji chao kushambuliwa na walitembea kilometa 200 kwa kuwa hawakua na fedha za kulipia ufadhili. Hapa wenyeji waliwapatia chakula n…
© UNICEF/Newson Hounkpatin
Wazazi wa Abasse, Ousséni Dahani na Ramatou Yonli wakiwa nje ya nyumba yao huko Benin. Walikimbia Burkina Faso baada ya kijiji chao kushambuliwa na walitembea kilometa 200 kwa kuwa hawakua na fedha za kulipia ufadhili. Hapa wenyeji waliwapatia chakula na maji na pahala pa kulala.

UNICEF inasema mapigano yanazidi kuwa ya kikatili ambapo baadhi ya vikundi vilivyojihami vinaendesha operesheni zao katika maeneo ya Mali, Burkina Faso na Niger ambako wanatumia mbinu kama vile kuweka vizuizi mijini na vijijini na hata kuharibu mitandao yam aji.

Kama hiyo haitoshi, UNICEF inasema kutokana na mashabulizi hayo zaidi ya watu 20,000 kwenye maeneo ya mpaka baina ya Burkina Faso, Mali na Niger watakuwa na kiwango cha kutisha cha ukosefu wa chakula ifikapo mwezi Juni mwaka huu.

Vikundi vilivyojihami ambavyo vinapinga elimu inayotolewa na serikali vinatia moto majengo ya shule na kupora mali, vinaweka vitisho, vinateka nyara au kuua walimu.

Zaidi ya shule 8,300 zimefungwa katika shule zote kwa sababu zilishambuliwa moja kwa moja na walimu kukimbia au kwa sababu wazazi walikimbia au wanahofia kupeleka watoto wao shuleni.

Sasa Abasse na familia yake wako Benin na akiwa darasani akiandika anasema “kwa kuwa sasa naenda shuleni, nimepata marafiki. Napenda kifaransa, nazungumza kidogo. Na mwalimu wangu ni mzuri.”

UNICEF inasema janga la Sahel ya Kati bado halijapata ufadhili wa kutosha kuweza kufanikisha operesheni zake kwani mwaka 2022 ilipokea theluthi moja tu ya dol amilioni 391 na kwamba mwaka huu imeomba dola milioni 473 kufanikisha operesheni za kiutu Sahel ya Kati na nchi Jirani.