Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tuwekeze ili kila mtu popote alipo apate chakula bora- Guterres 

Watoto wa shule wakipata mlo shuleni uliopikwa kwa mboga mboga mbazo kutokana na umbo lake hakifuaa soko ya nje
WFP/Martin Karimi
Watoto wa shule wakipata mlo shuleni uliopikwa kwa mboga mboga mbazo kutokana na umbo lake hakifuaa soko ya nje

Tuwekeze ili kila mtu popote alipo apate chakula bora- Guterres 

Masuala ya UM

Leo ni siku ya chakula duniani ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema ushindi wa tuzo ya amani ya Nobel kwa shirika la mpango wa chakula la Umoja wa Mataifa, WFP ni utambuzi wa haki ya chakula kwa kila mtu na azma ya pamoja ya kutokomeza njaa duniani.

Kauli mbiu ya siku hii ikiwa ni Otesha, Stawisha, Endeleza kwa Pamoja; Vitendo Vyetu Mustakabali wetu! Guterres anasema cha kustaajabisha ni kwamba katika dunia yenye utajiri, bado kuna mamilioni ya watu wanaolala njaa kila usiku. 

Hali imekuwa mbayá zaidi wakati wa sasa wa janga la ugonjwa wa Corona, COVID-19 ambalo limezidi kuongeza kiwango cha njaa na ukosefu wa chakula ambao haujawahi kushuhudiwa miongo kadhaa. “Takribani watu milioni 130 wako hatarini kutumbukia kwenye njaa mwishoni mwa mwaka huu hii ikiwa ni nyongeza ya watu wengine milioni 690 ambao tayari hawana mlo. Na wakati huo huo zaidi ya watu bilioni 3 hawawezi kumudu mlo wenye afya,”  

Kutokana na COVID-19, mizozo ya vita na hata mabadiliko ya tabianchi, mamilioni ya watu wanategemea msaada wa chakula ambapo WFP husambaza kwa njia mbalimbali ikiwemo kurusha angani, huku shirika la chakula na kilimo duniani ambalo leo linatimiza miaka 75, linapatia wakazi wa dunia stadi bora za kilimo endelevu na cha kuhakikisha upatikanaji wa chakula. 

Ni kwa mantiki hiyo Katibu Mkuu Guterres anasema,"Hatuna budi kuimarisha juhudi zetu za kufanikisha dira ya malengo ya maendeleo endelevu, SDGs. Hii ina maana kuwa na mustakabali ambamo kwao kila mtu, kokote pale aliko anapata lishe bora anayohitaji. Tunahitaji kuhakikisha mifumo ya chakula ina mnepo dhidi ya hatari zozote na pia mabadiliko ya tabianchi. Tunahitaji kuhakikisha kila mtu anapata lishe bora na tupunguze utupaji wa chakula. Inahitajika mifumo ya chakula ambayo itanweza kupatia wafanyakazi mbinu za kujipatia kipato ambazo ni salama na zenye utu.” 

Amekumbusha kuwa dunia hivi sasa ina teknolojia na uwezo wa kuunda dunia endelevu zaidi, yenye usawa na mnepo kwa hiyo katika siku ya leo kila mtu aweke ahadi ya kukuza, kustawisha na kuendeleza kwa pamoja.