Kushughulikia afya ya akili ni muhimu katika kufikia uhakika wa afya kwa wote-Guterres  

9 Oktoba 2020

Kuelekea siku ya afya ya akili inayoadhimishwa kesho Oktoba 10, huku takwimu zikionesha kuwa takribani watu bilioni 1 duniani kote wanaishi na matatizo ya akili, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kupitia ujumbe wake kwa siku hii amesema, inabidi hatua zichukuliwe ili kuhakikisha kunakuwa na huduma bora ya afya ya akili kwa wote kwani hivi sasa inaonesha pia kuwa kila sekunde 30 mtu mmoja anajiua kutokana na tatizo hili la afya ya akili.  

“Sasa tunaona madhara ya janga la COVID-19 kwa ustawi wa akili za watu, na huu ni mwanzo tu. Makundi mengi, wakiwemo wazee, wanawake, watoto na watu wenye matatizo ya akili wako katika hatari ya kudhoofika kiafya kwa kipindi cha muda wa kati na mrefu ikiwa hatua hazitachukuliwa.”  Amesema Guterres

Bwana Guterres ameeleza kuwa ni watu wachache mno ambao wanapata huduma bora ya afya akiongeza kuwa katika nchi za kipato cha chini na cha kati, zaidi ya asilimia 75 ya watu wenye matatizo ya akili hawapati kabisa matibabu na kiujumla serikali zinatumia chini ya asilimia mbili ya bajeti zao za afya kushughulikia suala la afya ya akili, na hilo halipaswi kuendelea, “hatuwezi kupuuza tena hitaji la kuongeza kiwango kikubwa katika uwekezaji katika afya ya akili. Lazima tuchukue hatua kwa pamoja, sasa, ili kutoa huduma bora ya afya ya akili kwa wote wanaohitaji ili kuturuhusu kupona haraka kutoka katika janga la COVID-19." 

 

 

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter