Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wahamiaji wengi toka Afrika hawaendi Ulaya wala Amerika bali katika nchi za Afrika:IOM/AUC Ripoti 

Wahamiaji kutoka Guinea wakiwa wamewasili nchini Libya.
IOM
Wahamiaji kutoka Guinea wakiwa wamewasili nchini Libya.

Wahamiaji wengi toka Afrika hawaendi Ulaya wala Amerika bali katika nchi za Afrika:IOM/AUC Ripoti 

Amani na Usalama

Ripoti mpya na ya kwanza kabisa ya uhamiaji Afrika iliyotolewa na shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM na tume ya Muungano wa Afrika AUC, imebaini kwamba wahamiaji wengi wa bara hilo hawaendi kwingineko bali barani mwao Afrika.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyopewa jina “Uhamiaji Afrika, kukabiliana na dhana iliyopo”, katika karne hii ya 21 uhamiaji barani Afrika unafanyika kwa njia ya barabara na sio baharini, na maeneo wanakokwenda wahamiaji hao kwa wingi sio Ulaya wala Amerika ya Kaskazini  bali ni ndani ya nchi za Afrika. 

Hayo ni baadhi ya matokeo ya utafiti wa ripoti hiyo ya kihistoria iliyowasilishwa kwenye mkutano kwa njia ya mtandao uliowaleta pamoja watunga sera, wataalam wa masuala ya uhamiaji na mashirika wadau wa Umoja wa Mataifa. 

IOM na AUC wanasema lengo kubwa la ripoti hiyo ni kujaribu kubadili dhana ambayo imekuwepo kwa muda mrefu kuhusu uhamiaji katika bara la Afrika. 

Katika taarifa yake kwenye mkutano huo mkurugenzi mkuu wa IOM Antonio Vitorino amesema “Ripoti hii imekuwa muhimu zaidi kwetu kuisoma katika muktadha wa janga la COVID-19, na ina maana zaidi haswa ukizingatia kwamba sehemu kubwa ya uhamiaji wa Afrika unasalia ndani ya bara hilo. Inatukumbusha jinsi gani uhamiaji unavyohusiana na kila nyanja ya jamii zetu na uchumi. Na inasisitiza haja muhimu ya kujumuisha wahamiaji katika hatua zetu za kupambana na majanga katika sera zetu zote za umma. Na pia inatulazimisha kuangalia zaidi ya matatizo ya leo na kufikiria wapi changamoto na suluhu za kesho zitapatikana.” 

Naye kamishina Amira El Fadil kutoka AUC amelishukuru shirika la IOM akisema ushirikiano wao umeweka msingi wa kufanyia kazi sera za uhamiaji barani Afrika na kuongeza kuwa “Hii ni muhimu hasa wakati huu ambao bara la Afrika linapiga hatua kubwa katika utekelezaji wa masuala mengi ikiwemo biashara huria barani humo (AfCFTA) na kuufanyia kazi mkataba wa uhuru wa watu kutembea baina ya nchi za bara hilo.” 

Ripoti hiyo imesema hadithi za wahamiaji wa Afrika wakihaha kwenye boti kuvuka bahari ya Mediterranea kwenda Ulaya zimekuwa ndilo gumzo, na hili linapotosha uelewa wa umma, kwani ukweli ni kwamba asilimia kubwa ya wahamiaji wa Afrika wanasafiri kwa barabara na sio kuvuka bahari. 

Wataalam wa uhamiaji walioshiriki mkutano huo wamesema ripoti hii inatoa fursa muhimu kwa watunga sera za uhamiaji Afrika kutafakari maswali katika sera zao husuan baada ya janga la COVID-19.