Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ubakaji ni kosa lakini kuwahukumu kifo na kuwahasi watekelezaji si suluhu:Bachelet 

Wanaume nchini Liberia wakiandamana na mabango ya kupinga ubakaji
Photo: UNMIL/Staton Winter
Wanaume nchini Liberia wakiandamana na mabango ya kupinga ubakaji

Ubakaji ni kosa lakini kuwahukumu kifo na kuwahasi watekelezaji si suluhu:Bachelet 

Haki za binadamu

Kamishina mkuu wa haki za binadamu amesema ingawa watekelezaji wa ubakaji na mifumo mingine ya ukatili wa kingono lazima wawajibishwe, hukumu ya kifo au utesaji sio jawabu muafaka. 

Katika taarifa yake iliyotolewa leo mjini Geneva Uswis Michelle Bachelet ametoa wito kwa serikali kuongeza hatua dhidi ya uhalifu huo, kuboresha fursa za upatikanaji wa haki na fidia kwa waathirika na taasisi zifanye haraka uchunguzi na kuwashitaki wahusika. 

Chuki na wito wa kupata haki 

Tamko hilo la kamishina mkuu limekuja baada ya ripoti za hivi karibuni za vitendo vya ubakaji mbaya zaidi kwenye maeneo mbalimbali duniani ikiwemo Algeria, Bangladesh, India, Morocco, Nigeria, Pakistan na Tunisia. Vitendo hivi vimezua gadhabu na madai ya kupatikana kwa haki. 

“Naungana na gadhabu hizo na kusimama Pamoja na waathirika na wale wanaodai haki. Lakini ninatiwa hofu kwamba pia kuna wito na katika baadhi ya maeneo sheria tayari zimeshapitishwa za kutekeleza adhabu za kikatili na zisizo ubinadamu na pia hukumu ya kifo kwa wahalifu hao.” Amesema Bi. Bachelet 

Kuhasi na hukumu ya kifo 

Kasmisha mkuu ametoa mfano wa sheria hizo kama vile mabadiliko ya sheria yaliyopitishwa mwezi uliopita katika jimbo la Kaduna Kaskazini Magharibi mwa Nigeria. 

Amesema sheria hiyo inaruhusu wanaume wabakaji kuhasiwa na wanawake wanaohukumiwa kwa kosa hilo kuondolewa mirija yao ya uzazi. Na hatua hizo zitafuatiwa na hukumu ya kifo endapo muathirika wa ubakaji alikuwa chini ya umri wa miaka 14. 

Mapema wiki hii serikali ya Bangladesh imeidhimisha marekebisho ya sheria ambayo sasa yatatoa hukumu ya kifo kwa wabakaji, huku Pakistan kumekuwa na wito wa kuwanyonga hadharani na kuwahasi wabakaji. Ameongeza kuwa madai kama hayo ya hukumu ya kifo pia yamefanywa katika maeneo mengine. 

Fursa ya kupata haki ni muhimu 

Bi. Bachelet amesema wakati sababu kuu ya kutoa hukumu ya kifo katika suala hili ni Imani kwamba itakomesha ubakaji, ukweli ni kwamba hakuna Ushahidi wa kuunga mkono dhani hiyo. 

“Ushahidi unaonyesha kwamba uhakika wa adhabu badala ya ukali wake unazuia uhalifu. Katika nchi nyingi duniani tatizo kubwa ni kwamba waathirika wa ukatili wa kingono hawana fursa za kupata haki, ama ni kwa sababu ya unyanyapaa, hofu ya kulipiza kisasi, mila zinazobagua jinsia na kutokuwa na mamlaka, ukosefu wa polisi na mafunzo ya kutoa haki, sheria zinazounga mkono au kutoa msamaha kwa baadhi ya aina za ukatili wa kingono au kukosekana kwa ulinzi kwa waathirika. 

Jukumu kubwa la wanawake 

Kamishina Mkuu amesisitiza kwamba hukumu ya kifo au adhabu kama kuhasiwa au kuondolewa mirifa ya uzazi hakutotatua vikwazo vyovyote vya fursa za kupata haki wala hakutozuia vitendo hivyo. 

“Ukweli ni kwamba hukumu ya kifo ya mara kwa mara inabaguadhidi ya masikini na watu waliotengwa na mara nyingi inapelekea ukiukwaji zaidi wa haki za binadamu. Na kitendo cha kuwahasi au kuwatoa mirija ya uzazi kinakiuka sheria za kimataifa za haki za binadamu.” 

Kwa mantiki hiyo “Natoa wito kwa nchi kuchukua mtazamo wa kuwaangalia waathirika zaidi kupambana na jinamizi hilo la ubakaji na ukatili mwingine wa kingono. Ni muhimu kwa wanawake kuwa washiriki katika kuandaa hatua za kuzuia na kushughulikia uhalifu hu una kwamba maafisa wa usalama na wa masuala ya haki wapewe mafunzo muhimu ya kushughulikia kesi hizo.” Ameongeza Bi. Bachelet. 

Amesisitiza kwamba “Pamoja na hamasa ya kutaka kuwaadhibi vikali wanaotekeleza uhalifu huo mbaya Zaidi, tusituhusu sisi wenyewe kutekeleza ukiukwaji zaidi wa haki za binadamu.”