Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu
Robo ya visa vya ukatili wa kingono nchini Sudan Kusini ni dhidi ya watoto.

Viongozi Sudan Kusini wanawajibika kutokomeza ubakaji kwa wanawake na wasichana:UN tume 

© UNICEF/Mackenzie Knowles-Coursin
Robo ya visa vya ukatili wa kingono nchini Sudan Kusini ni dhidi ya watoto.

Viongozi Sudan Kusini wanawajibika kutokomeza ubakaji kwa wanawake na wasichana:UN tume 

Haki za binadamu

Wanawake na wasichana wanaendelea kuishi maisha ya jehanamu nchini Sudan Kusini kutokana na unyanyasaji na ukatili ukiwemo wa kingono unaofanywa na makundi yote yenye silaha katika mzozo unaondelea nchini humo, imesema ripoti mpya iliyotolewa leo na tume ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Kibinadamu nchini humo.   

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ubakaji ulioenea, mara nyingi hufanyika kama sehemu ya mbinu za kijeshi ambazo viongozi wa serikali na kijeshi wanawajibika, ama kutokana na kushindwa kwao kuzuia vitendo hivi, au kwa kushindwa kwao kuwaadhibu waliohusika.   

Yasmin Sooka mwenyekiti wa tume hiyo amesema, "Inachukiza na haikubaliki kabisa kwamba miili ya wanawake inatumiwa kiholela katika kiwango hiki kama mbinu za vita. Hatua za haraka na zinazoweza kukomesha ukatili kutoka kwa mamlaka zimechelewa mno, na wanaume wa Sudan Kusini ni lazima wakome kuichukulia  miili ya wanawake kama  chombo cha kumilikiwa, kudhibitiwa na kunyanyaswa."  

Ushahidi na waathirika 

Ripoti hiyo inatokana na mahojiano yaliyofanywa na waathiriwa na mashahidi kwa miaka kadhaa. 

Ripoti imeainisha kwamba manusura wameeleza kwa kina ubakaji wa kikatili na wa muda mrefu wa magenge unaofanywa dhidi yao na wanaume wengi, mara nyingi huku waume zao, wazazi au watoto wao wakilazimika kushuhudia, bila msaada wa kuingilia kati.  

Wanawake wa rika zote wameelezea kubakwa mara nyingi huku wanawake wengine pia wakibakwa karibu nao.  

Mwanamke aliyebakwa na wanaume sita alisema hata alilazimishwa kuwaambia waliomshambulia kuwa ubakaji huo ulikuwa mzuri, la sivyo walitishia kumbaka tena.  

Athari za ukatili huo zinasababisha uharibifu mkubwa wa maisha ya kijamii. 

"Mtu yeyote anayesoma maelezo ya ripoti hii ya kutisha anaweza tu kuanza kufikiria jinsi maisha yalivyo kwa waathirika. Hadithi hizi kwa bahati mbaya ni ncha tu ya barafu. Kila mtu, ndani na nje ya serikali, anapaswa kufikiria nini anaweza kufanya ili kuzuia vitendo zaidi vya unyanyasaji wa kijinsia na kutoa msaada wa kutosha kwa manusura,” amesema Andrew Clapham, mjumbe wa tume hiyo 

Ripoti imeendelea kusema kwamba wanawake wa Sudan Kusini wkati mwimngine hupigwa na kuumizwa kimwili wakati wakibakwa kwa mtutu wa bunduki, na mara nyingi hushikiliwa na wanaume huku wakinyanyaswa na wengine.  

“Wanaambiwa wasipinge hata kidogo, na wasiripoti kilichotokea, au watauawa. Mwanamke mmoja alieleza kuwa rafiki yake alibakwa na mwanamume mmoja msituni kisha akasema alitaka kuendelea kuburudika na kuendelea kumbaka kwa kutumia kuni iliyomsababisha kuvuja damu hadi kufa. “ 

Wasichana vigori walielezea kuachwa wakidhaniwa kuwa wamekufa na wabakaji wao huku wakivuja damu nyingi.  

Wahudumu wa afya wanasema walionusurika wengi wamebakwa mara nyingi katika maisha yao yote. 

Athari za ubakaji ikiwemo watoto wasiotarajiwa  

Ripoti hiyo inaelezea kuwa wanawake mara nyingi huzaa watoto kutokana na ubakaji, na inabainisha kuwa mara nyingi waathirika wameambukizwa magonjwa ya zinaa ikiwa ni pamoja na VVU.  

Wanawake wameachwa na waume na familia, na kuachwa maskini. Baadhi ya wale waliobakwa wakiwa wajawazito walipoteza mimba. 

Waume wanaotafuta wake na mabinti waliotekwa nyara mara nyingi hutumia miaka mingi bila kujua hatima yao.  

Baadhi waligundua kuwa walitekwa nyara na wanaume kutoka makabila hasimu na kulazimishwa kuzaa watoto wengi , mathalani mtu mmoja kama huyo alikuwa ameumizwa sana na alitaka kujiua. 

Tume imegundua kuwa mashambulizi haya hayakuwa matukio ya bahati nasibu, lakini kwa kawaida yalihusisha askari wenye silaha wakiwasaka wanawake na wasichana.  

Ubakaji unaofanywa wakati wa mashambulizi dhidi ya vijiji ni wa utaratibu na umeenea. 

Tume imesema kushindwa kwa wasomi wa kisiasa kushughulikia mageuzi ya sekta ya usalama, na kutoa mahitaji ya kimsingi ya vikosi vya kijeshi kutoka pande zote, kunachangia katika mazingira ya kuruhusu wanawake wa Sudan Kusini kuchukuliwa kama sarafu. 

Ukwepaji wa sheria na kutowajibika 

Kutokuadhibiwa kwa karibu vitendo vyote vya ubakaji na unyanyasaji wa kijinsia kunafanya kusiwe na uwezekano mkubwa kwamba wahalifu watawahi kuwajibika.  

Kwa mujibu wa ripoti uhalifu huu wa kutisha katika migogoro hufanyika katika muktadha wa mfumo dume na ukosefu wa usawa wa kijinsia.  

Nusu ya wanawake wote wa Sudan Kusini wameolewa wakiwa chini ya umri wa miaka 18, na nchi hiyo ina kiwango cha juu zaidi cha vifo vya uzazi duniani.  

"Inatia kashfa viongozi wakuu wanaohusishwa na ukatili dhidi ya wanawake na wasichana wakiwemo mawaziri na wakuu wa mikoa, hawaondolewi mara moja madarakani na kuwajibishwa. Ili kukabiliana na ukatili huu uliokithiri katika migogoro na mazingira mengine, walio katika nyadhifa za makamanda na mamlaka nyinginezo. Ni lazima na muhimu mara moja na hadharani kupitisha sera ya kutovumilia dhidi ya unyanyasaji wa kingono na kijinsia." Amesema Barney Afako, mjumbe mwingine wa tume hiyo. 

Tume imetoa wito kwa mamlaka nchini Sudan Kusini kuchukua hatua zinazohitajika kukomesha unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya wanawake na wasichana, kwa kushughulikia hali ya kutokujali na vichochezi vya migogoro na ukosefu wa usalama.  

Ripoti hiyo inahitimisha kwa mapendekezo ya jinsi ya kukabiliana na hali hiyo.