Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Lengo la kudhibiti kifua kikuu(TB) hatarini kutotimia:WHO Ripoti

Daktari nchini India akichunguza vipimo vya x-ray vya mgonjwa kwa ajili ya maambukizi kwenye mapafu
© UNICEF/Vinay Panjwani
Daktari nchini India akichunguza vipimo vya x-ray vya mgonjwa kwa ajili ya maambukizi kwenye mapafu

Lengo la kudhibiti kifua kikuu(TB) hatarini kutotimia:WHO Ripoti

Afya

Ripoti mpya iliyotolewa leo na shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO imeonya kwamba endapo uwekezaji na hatua za haraka hazitochukuliwa malengo ya kuzuia na kutibu kifua kikuu au TB huenda yasitimie mwaka 2022.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo kabla ya janga la corona au COVID-19, nchi nyingi zilikuwa zinapiga hatua katika vita dhidi ya TB, maambukizi yakipungua kwa asilimia 9 kati ya mwaka 2015 na 2019 na idadi ya vifo ikishuka kwa asilimia 14 katika kipindi hichohicho. 

Pia imesema utashi wa kisiasa wa viongozi wa kitaifa na kimataifa ulikuwa unazaa matunda. Hata hivyo ripoti hiyo mpya inaonyesha kwamba fursa za huduma za kifua kikuu zimesalia kuwa ni changamoto na kwamba malengo ya kuzuia na kutibu huenda yasifikiwe bila hatua madhubuti. 

Takwimu za WHO zinaonyesha kwamba takribani watu milioni 1.4 walikufa kutokana na magonjwa yanayohusiana na TB mwaka 2019, na katika watu milioni 10 waliokadiriwa kuugua TB mwaka jana, milioni 3 kati yao hawakupimwa ugonjwa huo au hawakuorodheshwa rasmi katika mamlaka husika. 

Mkurugenzi mkuu wa WHO Dkt.Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema “Fursa sawa za vipimo vyenye ubora na kwa wakati, hatua za kuzuia, matibabu na huduma kwa wagonjwa bado ni changamoto kubwa. Hatua za kasi na za haraka zinahitajika duniani kote endapo tunataka kufikia malengo ya 2022.” 

Kwa mujibu wa ripoti watu wapatao milioni 14 walitibiwa TB kati ya mwaka 2018-2019 idadi ambayo ni zaidi kidogo ya theluthi moja ya watu milioni 40 wanaotakiwa kutibiwa katika mkakati wa miaka mitano wa kuanzia 2018-2022.

Ripoti inasema changamoto kubwa ni fedha za kufadhili, mikakati ya kuzuia, upimaji, matibabu na huduma kwa wagonjwa wa kifua kikuu. Azimio la kisiasa lililopitishwa na viongozi wa dunia kwenye Umoja wa Mataifa liliweka lengo la dola bilioni 13 kwa ajili ya kufikia malengo ya TB lakini hadi sasa fedha zilizopatikana ni dola bilioni 6.5 ambazo ni nusu ya lengo. 

Pia ripoti imesema“Kuvurugwa kwa huduma za TB kulikosababishwa na janga la COVID-19 kumeongeza pigo katika vita hivyo. Katika nchi nyingi rasilimali watu, fedha na nyingine muhimu zimehamishwa kutoka kwenye vita dhidi ya TB na kuingizwa kwenye vita dhidi ya COVID-19, na hivyo kuathiri pia ukusanyaji wa takwimu na mifumo ya kuripoti kuhusu kifua kikuu.” 

Hata hivyo kufuatia mwongozo wa WHO, nchi zimechukua hatua kukabiliana na athari za COVID-19 katika huduma muhimu za kifua kikuu ikiwemo kuimarisha udhibiti wa maambukizi na kutumia teknolojia ya kidijitali kutoa huduma.