Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ulemavu unakuwa kulemaa kutokana na fikra za watu: Djenalib Ba

Donata Nyirakaboozi, mkimbizi mwenye ulemavu wa kutoona anayesimulia changamoto alizokumbana nazo vitani nchini DRC
UN News/ John Kibego
Donata Nyirakaboozi, mkimbizi mwenye ulemavu wa kutoona anayesimulia changamoto alizokumbana nazo vitani nchini DRC

Ulemavu unakuwa kulemaa kutokana na fikra za watu: Djenalib Ba

Masuala ya UM

Watu bilioni 1 kote dunia wana ulemavu na asilimia 80 wanaishi katika nchi zinazoendelea wakikabiliwa na changamoto kubwa ikiwemo unyanyapaa, ubaguzi na kutopata fursa za kuwezesha kuchangia katika jamii kwa mujibu wa shirika la kimataifa la mpango wa maendeleo ya kilimo IFAD.  Nchini senegali mmoja wa watu wenye ulemavu ameamua kukabiliana na moja ya fikra potofu kwamba ulemavu ni kulemaa. Kulikoni? 

Djenalib Ba mwenye umri wa miaka 45 ni mlemavu wa miguu anasema tatizo la ulemavu wake halimsumbui kwani anajiona kuwa ni mtu mwenye uwezo wa kuchangia katika jamii kama wengine. 

Ba ambaye alizaliwa mzima kama watoto wengine alipata ulemu baada ya kuugua akiwa na umri wa miaka mitatu lakini hata siku moja hajaupa  ulemavu wake nafasi ya kumlemaza,“Nina karakana na wakati huohuo nimeajiri na ninatoa mafunzo kwa vijana watano. Ninatengeneza na kukarabati vifaa vya kilimo, pia tunatengeneza viti mwendo na hata magari au kusafisha mitambo, tulipewa mafunzo kwa ajili ya kazi hizi” 

Mafunzo hayo aliyapata kutoka kwenye jumuiya ya watu wenye ulemavu nchini Senegali ambayo inafadhiliwa na IFAD na ina wanachama zaidi ya 300, yakijumuisha stadi mbalimbali zikiwemo pia kilimo, utengenezaji wa sabuni, biashara na ufundi makenika. 

Mafunzo hayo yamewasaidia watu hawa wenye ulemavu kujikimu wao na familia zao kama anavyothibitisha Ba,“Nimejifunza taaluma, na kwa kazi hii nalisha familia yangu, watoto wangu wote wanakwenda shule na mdogo kabisa yuko chekechea. Wakati mwingine nakuwa na uwezo zaidi ya watu wasio na ulemavu.” 

Djenalib anasema lengo lake kubwa ni kuidhihirishia jamii kwamba ulemavu sio kulemaa, bali fikra za watu ndio huwalemaza watu wenye ulemavu wakiamini kwamba hawawezi kufanya chochote fikra ambazo si sahihi.