Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Twasubiri nini kujumuisha watu wenye ulemavu kwenye nyanja zote?

Majanga yanapotokea, watu wenye ulemavu ndio wanapata shida zaidi kwa kuwa ni vigumu kujiokoa. Pichani ni nchini Syria mfanyakazi wa IOM akimsikiliza mtu mwenye ulemavu
IOM Syria
Majanga yanapotokea, watu wenye ulemavu ndio wanapata shida zaidi kwa kuwa ni vigumu kujiokoa. Pichani ni nchini Syria mfanyakazi wa IOM akimsikiliza mtu mwenye ulemavu

Twasubiri nini kujumuisha watu wenye ulemavu kwenye nyanja zote?

Masuala ya UM

Uchechemuzi thabiti unaoendelea hivi sasa wa haki za wanawake na wanaume wenye ulemavu katika nyanja zote ikiwemo michezo unaleta mabadiliko ya kudumu.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema hayo jijini New York Marekani wakati akihutubia mkutano wa 11 wa nchi wanachama wa mkataba wa kimataifa wa watu wenye  ulemavu.

Amesema nyanja ambazo zinafungua milango kwa kundi hilo ni pamoja na sayansi akisema itakuwa ni jambo jema kupanua wigo na fursa kwa ajili ya kundi hilo kwa kusaidia serikali.

“Tunahitaji kuimarisha mifumo yetu ya sera katika ngazi ya ushirikiano wa kimataifa kwa mujibu wa mkataba wa kimataifa wa haki za watu wenye ulemavu pamoja na malengo ya maendeleo endelevu, SDGs. Iwapo watu wenye ulemavu ni sehemu ya jitihada zetu za kufanikisha SDGs, tunapaswa kuhakikisha taasisi, mifumo na michakato ya kufanikisha hilo inakuwa inaratibiwa pamoja,” amesema Katibu Mkuu.

Bwana Guterres amesema suala hilo la kuratibu ndio litakuwa msingi wa ripoti yake ya kwanza kuhusu watu wenye ulemavu na maendeleo ambayo ataitoa baadaye mwaka huu.

Wakati hayo yakiendelea, Katibu Mkuu amesema ili kuhakikisha Umoja wa Mataifa unatekeleza kile ambacho inapigia chepuo, ameanzisha tathmini ya kina kuhusu kile ambacho chombo hicho inafanya katika kusongesha haki za watu wenye ulemavu.

Tathmini hiyo, kwa mujibu wa Bwana Guterres itaangalia ni jinsi gani Umoja wa Mataifa unashughulikia masuala ya ulemavu kuanzia miundombinu ya kuwezesha mienendo ya kundi hilo, ujumuishaji wa ajenda ya ulemavu katika kazi zote za chombo hicho hususan maendeleo na usaidizi wa kibinadamu.

“Kwa pamoja tunaweza kuondoa vizingiti na kuongeza uhamasishaji ili watu wenye ulemavu waweze kujumuika ipasavyo kwenye jamii na dunia nzima kwa ujumla,” amesema Katibu Mkuu.

Mkataba wa kimataifa wa watu wenye ulemavu, CRPD ulipitishwa mwaka 2006 na unalinda haki za watu bilioni 1.5 wenye ulemavu.

 

Image
Miundombinu bora huwezesha watu wenye ulemavu kushiriki hata kwenye mikutano inayojadili masuala yanayohusu mustakhbali wao. (Picha:UN/Kim Haughton)

Yaelezwa kuwa mkataba huo ni miongoni mwa mikataba ya haki za binadamu iliyoridhiwa na mataifa mengi zaidi ambapo hadi sasa nchi 177 wanachama wa Umoja wa Mataifa wameuridhia.

Kupitia mkataba huo, nchi hizo zinaazimia kulinda haki za watu wenye ulemavu katika jamii na kwamba haki zao zizingatiwe katika nyanja zote.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameseam kutia saini na kuridhia mkataba huo pekee haitoshi akisema kuwa “utekelezaji ni muhimu. Nchi lazima zitumie mkataba huo katika sera za maendeleo, uwekezaji na mifumo ya sheria iwapo tunataka kukidhi ahadi yetu ya msingi ya ajenda 2030 ya malengo ya maendeleo endelevu; kutokumwacha nyuma mtu yeyote.”