Miongoni mwa tulizokuwa nazo wiki hii
Watu wenye ulemavu wakumbukwe katika suala la utalii-Mbunge Tanzania. Mtu 1 kati ya 3 duniani hana fursa ya kupata maji safi ya kunywa na huduma za kujisafi- UNICEF/ WHO. Ili kukomesha ukatili wa ngono katika mizozo juhudi zaidi zahitajika:EU/UN. Matibabu ya kifafa bado ni shida kubwa kwa nchi za kipato cha chini- WHO. Nzige na Parara ndio chakula cha siku zijazo- Chef Ali
Watu wenye ulemavu wakumbukwe katika suala la utalii-Mbunge Tanzania

Mkutano wa 12 wa nchi wanachama wa mkataba wa haki za watu wenye ulemavu, CRPD, umefikia tamati wiki hii baada ya kudumu kwa wiki mbili wajumbe wakijadili masuala kadha kuhusu watu wenye ulemavu.
Mkutano huo ambao umefanyika katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani, umejikita zaidia katika kujadili mikakati ya kuhakikisha ahadi ya kutomwacha yeyote nyuma inatekelezwa.
Miongoni mwa washiriki ni Riziki Saidi Lulida, mbunge katika Bunge la Jamhuri ya muungano Tanzania ambaye alipaza sauti ya kuhakikisha watu wenye ulemavu hawaachwi nyuma katika sekta ya utalii.
Mtu 1 kati ya 3 duniani hana fursa ya kupata maji safi ya kunywa na huduma za kujisafi- UNICEF/ WHO

Ripoti mpya kuhusu pengo la usawa katika fursa ya kupata maji safi ya kunywa na masuala ya usafi na kujisafi inaonyesha kwamba zaidi ya nusu ya watu wote duniani hawana fursa ya kupata huduma salama za usafi.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyotolewa jumanne kwa ushirikiano wa shirika la afya duniani WHO, na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF, mabilioni ya watu duniani wanaendelea kutaabika kutokana na kukosa huduma bora za maji na masuala ya usafi.
Takribani watu bilioni 2.2 kote duniani, ripoti inasema hawana huduma ya maji salama ya kunywa, bilioni 4.2 wengine hawana huduma salama za usafi na watu bilioni 3 wanakosa huduma za msingi za sehemu za kunawa mikono.
Ili kukomesha ukatili wa ngono katika mizozo juhudi zaidi zahitajika:EU/UN

Muungano wa Ulaya na Umoja wa Mataifa kwa pamoja wamepaza sauti wakitaka jumuiya ya kimataifa kuongeza juhudi ili kukomesha mifumo yote ukatili wa kingono ikiwemo kutumika kama mkakati na mbinu za vita na ugaidi.
Kupitia ujumbe wao maalum kwa ajili ya siku ya kimataifa ya kutokomeza ukatili wa kingono katika migogoro Federica Mogherini mwakilishi wa ngazi ya juu wa Muungano wa Ulaya (EU) kwa ajili ya sera za mambo ya nje na Pramila Patten mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu uaktili wa kingono katika mizozo wamesema “ukatili wa kingono katika mizozo ni ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu ulio na athari mbaya za kimwili, kisaikolojia na kijamii, zinazoathiri maendeleo ya kiuchumi , mshikamano wa kijamii na amani na usalama wa kudumu.”
Matibabu ya kifafa bado ni shida kubwa kwa nchi za kipato cha chini- WHO

Robo tatu ya watu walio na ugonjwa wa kifafa katika nchi zenye kipato cha chini hawapati matibabu wanayoyahitaji na hivyo kuongeza hatari ya kufa kabla ya wakati wao, imesema ripoti mpya ya shirika la afya duniani WHO.
Ripoti inaendelea kueleza kuwa uwezekanao au hatari ya kifo cha mapema kwa watu wenye kifafa ni mara tatu zaidi kuliko kwa watu wasio na tatizo hilo ambapo katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati, vifo vya mapema miongoni mwa watu wenye kifafa ni vingi zaidi kuliko katika nchi zenye kipato kikubwa.
Nzige na Parara ndio chakula cha siku zijazo- Chef Ali

Umoja wa Mataifa kupitia shirika lake la chakula na kilimo FAO, limeanzisha kampeni ya kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha kuna uendelevu katika uzalishaji na ulaji wa chakula.
Lengo la kampeni hii iliyopatiwa jina #Actnow au chukua hatua sasa kwa kuzingatia mabadiliko ya tabianchi na ongezeko la watu duniani, inasaka kuhakikisha kuwa chakula kilichopo au kitakachozalishwa siyo tu kitatosheleza mahitaij ya kizazi cha sasa na kijacho bali pia kitakuwa ni chakula salama kwa afya ya mlaji.
Kupitia kampeni hiyo, FAO imeungana na wapishi wakuu kutoka maeneo mbalimbali duniani ili kuifanikisha azma hiyo.