Kambare wageuka kichocheo cha uchumi kwa wanawake wa Ibadan Nigeria 

6 Oktoba 2020

Mradi wa FISH4ACP ambao una lengo la kuimarisha uvuvi na ufugaji samaki barani Afrika, Karibea na Pasifiki ukifadhiliwa na shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa FAO, umesaidia kuinua uchumi kama anavyoeleza mmoja wa wanufaika nchini Nigeria Bi Yahya Olunbumi.

Ni katika mji wa Ibadan, wa tatu kwa wingi wa watu nchini Nigeria ambako Yahya Olunbumi alianza biashara ya ufugaji samaki aina ya kambare katika mazingira ambayo wengi walimuuliza kama yeye kwa kuwa ni mwanamke ataimudu kazi hiyo ambayo kwa kiasi kikubwa mnyororo wake wa thamani umehodhiwa na wanaume.  

Hivi sasa Bi Olunbumi anamiliki shamba lenye mabwawa yaliyosheni kambare katika nchi hiyo ambayo ndio wazalishaji wakubwa duniani wa aina hiyo ya kambare wa kiafrika.  

Mradi wa FISH4ACP unasaidia juhudi za Nigeria kukuza sekta ya samaki aina ya kambare kwa sababu ya uwezo wake wa kutengeneza nafasi za ajira na biashara, haswa kwa wanawake na vijana ambapo kwa fursa hiyo, Bi Olunbumi amefanikiwa kuwaajiri wanawake wenzake kama anavyoeleza,“asilimia 90 ya wafanyakazi wangu ni wanawake. Na kwa nini hivyi? Kwasababu baadhi ya wanaume wanahisi tuseme wanajisikia kudhalilika au hawataki kufanya kazi na wakisema kuwa huyu ni mwanamke.” 

Bi Olunbumi anasema zaidi ya asilimia 40 ya protini wanayokula nchini Nigeria inatokana na samaki. Soko ni kubwa na kimsingi bado kuna upungufu wa kiasi kinachohitajika kwasababu bado wanamalazimika kuagiza samaki kutoka nje. Kwa hivyo anasema angependa wawe na kitu kama duka moja ambapo wanawake ambao wako katika ufugaji mdogo wa samaki wanaweza kuja na samaki wao waliosindikwa na kuwe na kiwango fulani cha ubora ili waweze kupenya katika masoko mengine, "ninazungumzia kuhusu kuwa na jumuiya ya  kuchakata samaki, ambapo wanawake wote wanashiriki katika ufugaji wa samaki au usindikaji samaki na wanaweza kuja na bidhaa zao na kuuza katika katika soko lililo tayari.”  

Mfanyabiashara huyo anasema hivi sasa ana uwezo wa kuzalisha hadi tani tano za samaki kambare kwa mwaka.  

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter