Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nataka na mimi siku moja niitwe “Nellie mmiliki wa duka la kuoka mikate” 

Studio ya Redio Okapi huko Bukavu ilifungua milango yake kwa wanafunzi kama sehemu ya ziara iliyoongozwa ya MONUSCO. Wanafunzi hawa, wenye umri wa miaka 2 hadi 11, waliweza kugundua na kuelewa jukumu na dhamira ya MONUSCO, DRC.
MONUSCO/Alain Likota
Studio ya Redio Okapi huko Bukavu ilifungua milango yake kwa wanafunzi kama sehemu ya ziara iliyoongozwa ya MONUSCO. Wanafunzi hawa, wenye umri wa miaka 2 hadi 11, waliweza kugundua na kuelewa jukumu na dhamira ya MONUSCO, DRC.

Nataka na mimi siku moja niitwe “Nellie mmiliki wa duka la kuoka mikate” 

Ukuaji wa Kiuchumi

Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, mradi ulioendeshwa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF umewezesha watoto kufungua mradi wao wa kuoka na kupika mikate, mandazi na kalmati na hivyo kuona angalau nuru ya maisha kwenye taifa hilo lililogubikwa na mizozo hususan mashariki mwa nchi.

Tupo nje ya duka la kuoka mikate mjini Bukavu, jimboni Kivu Kusini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, tunakutana na Nellie mtoto mwenye umri wa miaka 14.  

Anasema akiwa darasa la 6, baba yake alifariki dunia baada ya kupigwa risasi mjini Uvira ambako alikuwa dereva. Mama yake hafanyi kazi na bibi yao ndio alikuwa na uwezo wa kusaka chakula, akipata wanakula akikosa wanalala njaa. Nuru iliingia akisema, “nilisikia kuhusu warsha ya mafunzo ya uokaji na hapo mambo yalibadilika. UNICEF ilisaidia kundi letu kwa mafunzo hayo na uanzishaji wa biashara. Tulijifunza pia kusoma na kuandika na jinsi ya kuoka mikate na kupika mandazi. Tulifanya mafunzo kwa vitendo. Mwishoni mwa mafunzo walitupatia fedha za kuanzisha biashara yetu. Licha ya kuwa na stadi za kuoka mikate, ilibidi tuanzishe kikundi lakini hatukuwa na jiko la kuoka.” 

Nellie waliingia ubia na wavulana watano ambao wazazi wo waliwasihi kuwa waishi kindugu na wasigombane. Miongoni mwao ni Tuishi mwenye umri wa miaka 13 ambaye anasema aliamua kuhamia Bukavu kwa matumaini kuwa kaka yake anaweza kumpeleka shule na pia angeweza kujipatia kipato baada ya shule. Tuishi anasema, “kila asubuhi naamka na tunapika mandazi 70 na pia wananipatia matano ya ziada ya kula. Kisha naenda kuuza. Mwisho wa wiki wananilipa ujira mdogo kwa kazi yangu. Natuma fedha nyumbani kusaidia mama yangu na pia ninapohitaji makubazi mapya naweza kujinunulia.” 

Wakati ndoto ya Tuishi ni siku moja aweze kupia mwenyewe mandazi, Nellie yeye pamoja na kufurahi kuwa na stadi hiyo mpya anasema,“Umoja ni muhimu. Kwa hiyo kila siku nasali ili tusalie kitu kimoja na siku moja tuwe na biashara yetu wenyewe. Kama vile ambavyo mtu atakutambua kwa kuwa mke au waziri, basi napenda siku moja wanitambue kuwa Nellie mmiliki wa duka la uokaji.”