Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Unapobakwa tambua huna kosa ila ni muathirika:Dkt.Mukwege

Dkt. Denis Mukwege, muasisi na mkurugenzi wa tiba wa hospitali ya Panzi huko DR Congo, wakati uzinduzi wa ripoti ya kamisheni ya kimataifa kuhusu afya jijini New York, Marekani 20 Septemba 2016
UN/JC Mcllwaine
Dkt. Denis Mukwege, muasisi na mkurugenzi wa tiba wa hospitali ya Panzi huko DR Congo, wakati uzinduzi wa ripoti ya kamisheni ya kimataifa kuhusu afya jijini New York, Marekani 20 Septemba 2016

Unapobakwa tambua huna kosa ila ni muathirika:Dkt.Mukwege

Afya

Ubakaji unasalia kuwa moja ya uhalifu mbaya zaidi duniani na cha kusikitisha ni kwamba asilimia kubwa ya waathirika hushindwa kujitokeza au kushitaki uhalifu huo wakidhani kuwa ni makosa yao.

Kauli hiyo imetolewa na Dkt. Denis Mukweke mmoja wa mataktari bingwa wa masuala ya wanawake nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, alipozungumza na UN News na kuwataka waathirika wa uhalifu huo kutambua kwamba hilo si kosa lao.

"Kwa kupinga ubakaji, tunahitaji zaidi. Kwanza, wanawake ambao wanapitia ubakaji, hata wanaume, wawe na uwezo wa kujua kwamba wao hawana kosa. Yule ambaye anakuwa na kosa ni yule ambaye amebaka. Hiki ni kitu cha kwanza cha muhimu kujua. Cha pili, ikiwa huna kosa, ni lazima umshitaki yule ambaye ametenda kitendo ambacho hakikubaliwi na sheria. Kwa sababu, ikiwa unanyamaza au unamficha, ni kusema unamsaidia kuendelea kufanya hiki kitendo kibaya si kwako tu, lakini na kwa wengine. Lakini kwa kujikinga wewe binafsi, na kukinga wengine, ni lazima kushitaki."

Dkt. Mukwege ambaye tangu 1999 amekuwa akifanya upasuaji katika hospitali ya Panzi  iliyoko Bukavu kurekebisha mauambile ya sehemu za siri kwa maelfu ya wanawake walioathiriwa na ubakaji kutokana na vita vinavyoendelea DRC amesisitiza umuhimu wa sheria katika hili

"Cha tatu, ni lazima kupinga impunity, au kufanya hata sheria iheshimike. Ikiwa kitendo cha ubakaji kinafanyika ni lazima huyo aliyekitenda aende mahakamani na akiri juu ya ile amekitenda. Ikiwa hatupingi impunity, ni kusema tunakubali kitendo hiki cha ubakaji kuendelea.​​​​​​"