Chonde chonde saidieni wanawake wanaobakwa na msisahau watoto wao wasio na utaifa- Dkt. Mukwege
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo lina mjadala wa wazi kuhusu ukatili wa ngono kwenye mizozo ikiwa ni miaka 10 tangu kupitishwa kwa azimio namba 1888 lililoanzisha wadhifa wa mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu kuhusu vitendo hivyo.
Miongoni mwa watakaohutubia kikao hicho ni mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel kwa mwaka 2018, Dkt. Denis Mukwege ambaye kupitia hospitali yake ya Panzi iliyoko mjini Bukavu,jimbo la Kivu Kusini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC amekuwa akitibu wanawake waliobakwa na vikundi vilivyojihami.
Idhaa ya Umoja wa Mataifa ilimuuliza Dkt. Mukwege nini ujumbe wake kwa Baraza la Usalama na amesema, “na ile ambayo tunaenda kuzungumzia zaidi ni kuomba kama Umoja wa Mataifa washughulike zaidi na wamama wanaopata shida ya ubakaji kwa nchi mbalimbali. Hii shida inahusu wamama na pia watoto ambao wanazaliwa kisha wamama wanabakwa. Hawa watoto ambao mara nyingi hawana taifa, hawana wazazi na wanatupiliwa, hii ni shida kubwa. Kitu cha tatu ni kuomba Umoja wa Mataifa ushughulike hata kama mama anapata shida ya ubakaji apate matunzo yanayomfaa, na apate kulipwa hii gharama ambayo ameipata kupitia ubakaji.
Msingi wa mjadala wa leo ni ripoti yam waka huu ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu ukatili wa kingono kwenye mizozo iliyotolewa tarehe 29 mwezi uliopita wa Machi.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa katika muongo mmoja uliopita, kumekuwepo na kubadilika kwa mwelekeo wa kuelewa ukatili wa kingono na uhusiano wake kwenye tishio la amani na usalama duniani.
“Wakati Umoja wa Mataifa unazidi kuimarisha operesheni zake za usalama na usaidizi wa kiufundi na kisheria ili kukabili ukatili wa kingono kwenye mizozo, bado ni muhimu kutambua umuhimu wa kushughulikia suala la ukosefu wa jinsia kama chanzo na kichocheo cha ukatili wa kingono,” imesema ripoti hiyo.
Kwa mantiki hiyo, Ujerumani ambayo ndio inashika uraisi wa Baraza la Usalama kwa mwezi huu wa Aprili, imeweka bayana kuwa msingi wa mjadala ni kuchambua mzizi wa ukatili wa kingono kwenye mizozo ikiwemo mtazamo na fikra potofu kuhusu ubaguzi wa kijinsia.