Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kutoka rejareja ya maziwa mgando hadi ukurugenzi wa kampuni kubwa DRC

ILO imejikita katika utoaji wa elimu ya ujasiriamali kwa wanawake na wanaume DR-Congo
ILO/screen capture
ILO imejikita katika utoaji wa elimu ya ujasiriamali kwa wanawake na wanaume DR-Congo

Kutoka rejareja ya maziwa mgando hadi ukurugenzi wa kampuni kubwa DRC

Ukuaji wa Kiuchumi

Kampeni ya kutomuacha mtu nyuma ya  shirika la Umoja wa Mataifa la ajira ILO,ambayo inawawezesha   vijana kukabiliana na changamoto za ajira imeanza kuzaa matunda nchiniJamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC, baada ya kutoa fursa kwa  baadhi ya vijana kujikwamua na umasikini

Miongoni mwa wanufaika ni Regina Kahindo ambaye kwa muda mrefu hakuwa na ajira kutokana na fani ya uuguzi aliyosomea haikumpa fursa ya kuajiriwa.

ILO kupitia makala iliyochapishwa kwenye wavuti wake inasema kuwa baada ya muda bila  ajira  Regina akapata wazo la kufanya biashara ili kujikwamua na umasikini akisema kuwa “Wazazi wangu walikuwa wanamiliki duka, kila mara tulikuwa tunaongelea kununua na kuuza bidhaa. Hivyo  wakati nasoma sikuweza kujizuia kufanya biashara zangu”

Regina akaanzisha biashara ndogo ya kuuza maziwa mgando chuoni kwake, ambayo ilipokelewa vizuri hadi baadhi ya wanafunzi wenzake walishtushwa na mafanikio aliyoyapata ndani ya muda mfupi.

“Kama wengine wanafanye na kufanikiwa, kwanini isiwe mimi?”alihoji Regina

ILO inasema kuwa biashara ya Regina ikapanuka, kwa mafanikio makubwa akiuza bidhaa zingine kama samaki,nyama ya nguruwe, mayai na mboga za majani.

Hata hivyo licha ya mafanikio, changamoto za ukosefu wa utaalamu na usimamizi wa biashara zikajitokeza na kumgharimu biashara zake na ndipo Regina aliposaka ushauri kutoka ILO kuhusu kuimairsha elimu ya usimamizi wa biashara.

“Nilifaidika sana na mafunzo yanayotolewa kulingana na mfumo wa biashara nchini hapa DRC,” amesema Regina.

Amina Maiga ambaye ni Mkurugenzi  wa ILO katika ofisi ya  Kinshasa nchini DRC amesema vijana wajasiriamali waliopatiwa mafunzo na shirika lake walitambulishwa na asasi za kidini na maendeleo ya vijana.

Akaongeza kuwa mafunzo waliyopewa  kutoka ILO yalijikita  katika misingi ya biashara akisema kuwa “utoaji wa mafunzo ya ujasiriamali kwa vijana nchini DRC unapewa kipaumbela sana.”

Baada ya mafunzo kutoka ILO, Regina sasa ni Mkurugezi Mtendaji wa kampuni yenye mafanikio nchini DRC iliyojikita na chakula na pia bidhaa za kujisafi za wanawake ambayo imewaajiri zaidi ya vijana 14.

Halikadhalika amejiotkeza kuwaelimisha vijana wengi nchini humo kutokana na uzoefu wake akisema kuwa "naanzisha maonyesho ya huduma kwa wajasiriamali wadogo ili kukuza sekta ya ndani ya DR Congo na hivyo kuwawezesha wajasiriamali wadogo kuendeleza masoko yao, kukutana na watumiaji na wawekezaji, kuboresha ubora wa bidhaa zao kwa kutumia mfumo wa tathmini ya watumiaji ili kuongeza tija.”