Wekeeni vikwazo wanaounga mkono wapiganaji mashariki mwa DRC- Rais Tshisekedi
Wekeeni vikwazo wanaounga mkono wapiganaji mashariki mwa DRC- Rais Tshisekedi
Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, Félix Tshisekedi amehutubia mjadala mkuu wa mkutano wa 75 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa akieleza kuwa janga la Corona, COVID-19 ambalo pamoja na kusababisha vifo, limekuwa kizingiti kikubwa kwa harakati mbalimbali duniani.
Akihutubia kwa njia ya video kutoka Kinshasa, nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, kupitia video iliyokuwa imerekodiwa awali, Rais Tshisekedi ametaja harakati zilizokwamishwa na COVID-19 kuwa ni pamoja na zile za kutokomeza umaskini, kusongesha amani na usalama na kusongesha maendeleo ya kijamii na ulinzi wa mazingira.
Hata hivyo amesema kuwa pamoja na kukabiliwa na janga hilo, kila nchi imekuwa mstari wa mbele kulinda raia wake na wakati huo huo kushirikiana na mataifa mengine kujifunza au kubadilisha uzoefu wa kukabili janga hilo.
“Mgonjwa wa kwanza wa Corona alipobainika jijini Kinshasa tarehe 10 mwezi Machi mwaka 2020, tulitangaza kuwa ni janga la kiafya la umma nchini lakini baada ya kuunda kikosi kazi cha kiserikali. Hata hivyo uzoefu wetu wa kukabiliana na Ebola umetusaidia kudhibiti ugonjwa huo,” amesema Rais Tshisekedi.
Amesema kuwa harakati za ndani sambamba na zile za kimataifa ikiwemo ushirikiano na wadau wa kimaendeleo na shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO, “zimesaidia kupunguza kiwango cha vifo visababishwavyo na COVID-19 kutoka asilimia 10 mwanzoni mwa janga hilo hadi chini ya asilimia 2.5 leo hii.”
Ukurasa kuhusu virusi vya Corona & Taarifa mpya
Wasomaji wanaweza kupata taarifa na muongozo kuhusu mlipuko wa virusi vya corona (2019-nCoV) kutoka Umoja wa Mataifa, Shirika la afya duniani na mashirika mengine ya UN hapa. Kwa habari mpya kila siku kutoka UN News, bofya hapa.Ametumia hotuba hiyo kusihi taasisi fedha za kimataifa kusamehe madeni bila masharti yoyote, kama njia mojawapo ili nchi maskini ziweze kujijenga upya baada ya COVID-19.
Amani na Usalama mashariki mwa DRC
Akizungumzia amani na usalama mashariki mwa nchi hiyo, Rais Tshisekedi amesema bado kuna masalia ya vikundi vilivyojihami ndani na nje ya nchi ambavyo vinaendeleza mashambulizi na kutia hofu kubwa. “Bado hakuna amani na vikundi hivyo siyo tu vinashambulia askari wetu, bali pia raia na walinda amani wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini DRC, MONUSCO ambao wanatupatia misaada mbalimbali ikiwemo vifaa.”
Amesema vikundi hivyo vinatekeleza ukatili mkubwa ikiwemo mauaji na ubakaji hususan Beni, Kivu Kaskazini na Njugu huko Ituri na Rutshuru.
“Tulichokiona kinadhihirisha kuwa vikundi hivi vina fedha za kuwawezesha kuendesha shughuli zao, na fedha hizo zinatokana na uporaji wa maliasili na kuziuza nje ya nchi kupitia mitandao mahsusi na bila shaka kwa msaada wa makundi fulani. Katu hatutaweza kusambaratisha hivi vikundi hadi pale tutakapoweza kusambaratisha mtandao huo na wale wanaowaunga mkono. Tunatoa wito kwa jamii ya kimataifa iweke vikwazo mahsusi vya kulenga makundi hayo na wale wanaowaunga mkono,” amesema Rais Tshisekedi.
MONUSCO kuondoka DRC?
Kuhusu mustakabali wa MONUSCO ni kwamba wakati huu wa maandalizi ya kuondoka kwa MONUSCO, ushirikiano kati ya ujumbe huo na jeshi la serikali uimarishwe ili kuhakikisha ulinzi endelevu wa raia hasa kwenye maeneo ambako bado vikundi vilivyojihami vimejiimarisha.