Ninajivunia kuiweka Marekani mbele, nanyi ndivyo mnapaswa kufanya kwa nchi zenu-Trump

22 Septemba 2020

Rais wa Marekani Donald Trump akiwa wa pili kuzungumza katika mjadala wa ngazi ya juu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa UNGA75, amesema anajivunia kuiweka Marekani mbele na ndivyo viongozi wengine wanapaswa kuziweka mbele nchi zao.  

Katika hotuba yake ya leo ambayo ilikuwa fupi kuliko wakati mwingine, ameisifia Marekani kwa namna mbalimbali kuanzia kupigania amani na haki za binadamu duniani na hata namna ilivyoshughulikia janga la ugonjwa wa COVID-19

Akianza na suala hilo la COVID-19, Rais Trump ameendelea kuishutumu China na kwamba nchi hiyo inapaswa kuwajibishwa kwa kuviruhusu virusi vya corona kusambaa duniani.  

“Katika siku za mwanzo za virusi, China ilifunga usafiri ndani ya nchi wakati ikiruhusu ndege kuondoka China kwenda kuambukiza dunia.” Amesisitiza Trump.  

Rais Trump akieleza namna Marekani ilivyofanya jitihada za kuidhibiti COVID-19 amesema kwa haraka walisambaza vifaa vya kusaidia kupumua, na pia wakatengeneza vya ziada kiasi cha kusambaza kwa marafiki na wadau wao kote duniani. Kuhusu chanjo dhidi ya virusi vya corona Trump amesema, “shukrani kwa juhudi zetu, chanjo tatu ziko katika hatua za mwisho za majaribio. Tunazizalisha nyingi kusudi zisambazwe zitakapowasili. Tutasambaza chanjo, tutavishinda vita, tutamaliza janga na tutaingia katika enzi mpya za ingiza enzi mpya ya mafanikio, ushirikiano na amani isiyokuwa ya kawaida.” 

Kuhusu suala la yeye kuiweka nchi yake ya Marekani mbele kuliko nchi nyingine yoyote, Trump amesema, “Kama Rais, nimekataa njia zilizoshindwa za zamani na ninajivunia kuiweka Amerika Kwanza, kama ambavyo mnapaswa kuweka nchi zenu kwanza. Hiyo ni sawa, ndivyo mnavyoapswa kufanya.”  

Kwa upande wa uchafuzi wa mazingira na hali ya hewa, Rais Trump hakuiacha China kwani ameendelea kuwashutumu na kutaka Umoja wa Mataifa kuwawajibisha kwani amedai nchi hiyo kila mwaka inatupa mamilioni ya tani za plastiki na takataka nyingine katika bahari, inavua samaki katika mipaka ya nchi nyingine, inaharibu matumbawe na kuachilia madini hatari ya mercury katika anga, zaidi kuliko nchi nyingine yoyote.  

“Hewa ya ukaa inayosambaza na China ni karibia mara mbili ya Marekani, na inazidi kuongezeka haraka.” Amesema Trump.  

Aidha Bwana Trump amesema Marekani itaendelea kuwa kinara wa haki za binadamu akisema kuwa uongozi wake unaendeleza uhuru wa kidini, fursa kwa wanawake, kupambana na mahusiano ya jinsia moja, kupambana na na usafirishaji haramu wa wat una kuwalinda watoto ambao hawajazaliwa.  

Kuhusu amani duniani ameeleza namna Mrekani inavyoendelea kushughulikia amani duniani kote akitolea mfano mashariki ya kati na kwingine akisema pia kuwa Marekani inasimama na watu wa Cuba, Nicaragua, na Venezuela katika harakati zao za haki za kupambania uhuru.  

 

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter