Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kwaheri UNGA74 karibu UNGA75

Volkan Bozkri, Rais wa mkutano wa 75 wa Baraza Kuu la UN, UNGA75 akinyanyua rungu kuashirikia kuchukua urais wa kiti hicho, huku Katibu Mkuu Antonio Guterres na Rais aliyemazali muda wake Tijjani Muhammad-Bande wakitazama.
UN WebTV
Volkan Bozkri, Rais wa mkutano wa 75 wa Baraza Kuu la UN, UNGA75 akinyanyua rungu kuashirikia kuchukua urais wa kiti hicho, huku Katibu Mkuu Antonio Guterres na Rais aliyemazali muda wake Tijjani Muhammad-Bande wakitazama.

Kwaheri UNGA74 karibu UNGA75

Masuala ya UM

Hatimaye mkutano wa 74 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa umefunga rasmi pazia lake hii leo na kuashiria kuanza kwa mkutano wa 75 wa Baraza hilo, ambalo ni moja vyombo vikuu vya Umoja wa Mataifa wenye wanachama 193.

 

Sherehe ya kufunga mkutano huo imefanyika ndani ya ukumbi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani na kuhudhuriwa na mabalozi wanaowakilisha nchi zao.

Akizungumza kwenye tukio hilo, Rais wa mkutano huo wa 74. Profesa Tijjani Muhammad-Bande amesema, “huu ni wakati wa kufikiria kuhusu sayari yetu ya pamoja na mustakabali wetu”  huku akipongeza vijana kwa uongozi wao wakati huu ambao dunia inakabiliwa na changamoto.

Profesa Muhammad-Bande ambaye anatoka Nigeria ameongeza kuwa huu in wakati wa kuchukua hatua, kuzingatia usawa, ujumuishi na ubia na kwa mantiki hiyo, “ni muhimu kwamba kazi za Umoja wa Mataifa zinaendelea kuhusisha vijana. Vijana wameonesha uongozi usio wa kawaida kwenye changamoto tunazokabili sasa duniani. Wamepaza sauti kwenye mabadiliko ya tabianchi, na usawa wa kijamii na hivyo ni lazima tusikilize sauti zao.”

Nani kapokea kijiti cha #UNGA75

Kijiti kimepokelewa na Volkan Bozkir, mwanadiplomasia kutoka Uturuki ambaye ataongoza mkutano wa 75 hadi mwezi Septemba mwakani.

Akila kiapo, Bwana Bozkir amesema, “ni wajibu wetu kuimarisha imani ya watu kwenye ushirikiano wa kimataifa na taasisi za kimataifa ambapo Umoja wa Mataifa ndio kitovu cha yote.”

Bozkir amesema “tunahitaji kusongesha mazungumzo ya wazi, ya dhati na yenye matokeo kuhusu kile kilichotokea katika harakati zetu za kudhibiti virusi vya Corona na kuepusha hali kama hiyo siku za usoni.”

Rais huyo wa mkutano wa 75 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ameongeza “tunahitaji kuuliza na kupata majibu kuhusu jinsi chanjo dhidi ya coronavirus">COVID-19 inaweza kusambazwa kwa usawa na kwa haki. Hii si hoja ya afya au uchumi, bali ni hoja ya maadili katika hali ya dhahiri kabisa.”

Rais wa mkutano wa 75 wa Baraza Kuu la UN, UNGA75, akizungumza na waandishi wa habari.
UN /Manuel Elias
Rais wa mkutano wa 75 wa Baraza Kuu la UN, UNGA75, akizungumza na waandishi wa habari.

Tukio la kufunga mkutano mmoja na kufungua mwingine hufanyika wiki moja kabla ya kuanza kwa mjadala wa wazi wa Baraza Kuu, mjadala ambao hufanyika mara moja kila mwaka na kuleta viongozi wa nchi na serikali kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani.

Hata hivyo kutokana na janga la COVID-19, mwaka huu, sehemu kubwa ya mjadala huo itafanyika kwa njia ya mtandao.

Akizungumza kwenye tukio la leo la kufunga mkutano wa 74 na kufungua wa 75, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema “kwa mjadala wa wazi kufanyika kwa kiasi kikubwa kimtandao, inamaanisha kwamba viongozi wengi zaidi wa nchi na serikali watashiriki wakati wa wiki hiyo, lakini bila shaka kwa kuwa ni mtandaoni kutakuwepo pia na changamoto. Itabidi tujifunze kadri siku zinavyosonga ili tuoneshe kuwa tunaweza kwenda na mazingira yalivyo.”

Katibu Mkuu ameongeza kuwa macho na masikio ulimwenguni kote ni kwa Umoja wa Mataifa kama jukwaa muhimu la ushirikiano wa kimataifa la kutatua changamoto za kimataifa.

Bila vikao vya uso kwa uso, kuna changamoto - Bozkir

Baada ya uzinduzi rasmi wa #UNGA75 Bwana Bozkir amezungumza na waandishi wa habari na kusema kuwa, “bila vikao vya uso kwa uso, sidhani kama Umoja wa Mataifa unaweza kufuatiliwa ulimwenguni kote. Tumaini langu ni kwamba kwa kuzingatia masharti ya tib ana kuheshimu kile ambacho wataalamu wa afya wanataka tufanye, basi tunaweza kuendelea na vikao vyetu vya uso kwa uso siku za usoni.”