Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mlipuko wa Ebola waendelea kusambaa  Equateur DRC na kuzusha hofu:WHO 

Watu kutoka shirika la msalaba mwekundu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wakitoa mafunzo kuhusu maziko salama katika kijiji cha Itipo(Juni 10, 2018)
WHO/Lindsay Mackenzie
Watu kutoka shirika la msalaba mwekundu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wakitoa mafunzo kuhusu maziko salama katika kijiji cha Itipo(Juni 10, 2018)

Mlipuko wa Ebola waendelea kusambaa  Equateur DRC na kuzusha hofu:WHO 

Afya

Mlipuko wa Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC sasa umesambaa zaidi katika maeneo mengine ya kanda 17 za jimbo la Equateur na hivyo kufanya jumla ya kanda za afya zilizoathirika kufikia 12. 

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva kwa njia ya mtandao, msemaji wa shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO, Fadela Chaib amesema maeneo yaliyoathirika hivi karibuni ni pamoja na Bomongo likiwa ni eneo la pili la kanda ya afya kuathirika ambalo linapakana na Jamhuri ya Congo hali ambayo inaongeza hofu ya kuzuka na kusambaa mlipuko huo wa ebola katika nchi nyingine. 

“Hii inafanya ushirikiano mpakani baina ya DRC na Jamhuri ya Congo kuwa ni wa muhimu zaidi sasa kuliko wakati mwingine wowote, na tutahitaji uratibu kuhusu ufuatiliaji wa ugonjwa huo na pia juhudi za kuwapima wasafiri. Hatari ya ugonjwa huo kusambaa hadi Kinshasa ipo na ni suala linalotutia hofu, kwani Mbandaka moja ya maeneo yaliyoathirika na mlipuko lina uhusiano na mji mkuu hasa kwa safari nyingi kupitia mtoni ambazo zinafanywa na maelfu ya watu kila wiki.”  Amesema Chaib.

Idadi ya wagonjwa 

Hadi kufikia Septemba 8 mwaka huu kulikuwa na visa 113 na 107 kati yao vimethibitishwa na 6 vikishukiwa, na watu 48 wameshapoteza maisha hadi sasa kwa mujibu wa WHO. 

Hata hivyo shirika hilo linasema katika habari njema, wagonjwa 52 wamepona na kuruhusiwa kwenda nyumbani kutoka katika vituo vya matibabu ya Ebola. Takribani watu 2431 waliokutana na wagonjwa wamefikiwa, kupimwa na watu 27,816 wamepatiwa chanjo dhidi ya Ebola

Hata hivyo hali imekuwa ngumu baada ya wahudumu wa afya kugoma na hivyo kuathiri hatua za kupambana na ugonjwa huo kwa karibu wiki nne. 

“Na ingawa shughuli hizo sasa zimeanza tena, lakini nyingi bado zimesismama na hivyo kufanya kuwa vigumu kupata picha halisi ya jinsi gani mlipuko huo unavyoendelea na maeneo gani yanayohitaji msaada Zaidi. Matumaini ni kwamba malipo ya mishahara yameanza wiki hii na tunatarajia kwamba operesheni zitaanza tena kama kawaida hivi karibuni.”  Ameongeza.

Licha ya changamoto, WHO na wadau wanaendesha kampeni kubwa ya uelimishaji katika jamii zilizoathirika. Wiki iliyopita pekee watu zaidi ya 80,000 wamejifunza kuhusu hatari za Ebola na jinsi ya kutambua dalili zake na kusaka matibabu. 

Changamoto za ufadhili  

WHO inasema jitihada za sasa za kupambana na mlipuko huo hazijafadhiliwa vya kutosha na hivyo kuongeza changamoto katika vikwazo vya kiufundi vilivyokuwepo. Awali shirika hilo lilitoa dola milioni 1.7 na kisha kuongeza zingine dola 600,000 kutoka fuko la dharura la WHO. 

Hivyo hii inafanya jumla ya fedha zilizopatikana kutoka kwa WHO kufikia dola milioni 2.3. Wizara ya afya ya DRC imewasilisha mkakati kwa wafadhili na wadau wengine ambao unahitajji dola milioni 40 na tayari wizara hiyo imetoa dola milioni 4. 

“Tunawaomba washirika kusaidia mkakati huu.Bila msaada wa ziada kwa timu inayopambana na Ebola mashinani itakuwa vigumu sana kuudhibiti mlipuko huu.” 

WHO imeongeza kuwa wakati huu ambapo janga la corona au coronavirus">COVID-19 likichukua asilimia kubwa ya rasilimali , kinachotakiwa ni kuongeza juhudi za kupambana na majanga yote mawili. COVID-19 sio dharura pekee inayohitaji msaada wa haraka. Na kama tunavyofahamu katika historia ya hivi karibuni tukipuuzia Ebola tunapuuzia kwa gharama yetu ambayo itakuwa kubwa zaidi.”  Limesisitiza shirika hilo la WHO.