Kasi kubwa ya kusambaa kwa Ebola jimboni Equateur nchini DRC yatia hofu WHO

21 Agosti 2020

Idadi ya wagonjwa wa Ebola kwenye jimbo la Equateur nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC imefikia 100, ikiwa ni ongezeko maradufu katika kipindi cha wiki 5.

Taarifa ya shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO iliyotolewa leo mjini Brazaville, Jamhuri ya Congo, imesema kuwa katika mlipuko huu wa 11 wa Ebola nchini DRC, uliotangazwa tarehe 1 Juni mwaka huu wa 2020, wagonjwa wa awali walibainika kwenye mji mkuu wa jimbo la Equateur, Mbandaka na sasa tayari Ebola imesambaa kwenye kanda 11 kati ya 17 za afya kwenye jimbo hilo.

Kati ya wagonjwa hao 100, 96 wamethibitishwa kuwa na Ebola ambapo kati yao hao 43 wamefariki dunia.
WHO inasema kuwa “mlipuko huu una changamoto kubwa katika kuwasilisha vifaa kwa wahusika kwa sababu eneo lenyewe liko katika msitu mnene, na jamii zimetawanyika katika eneo kubwa la takribani kilometa 300 kaskazini, mashariki, kusini na magharibi. Inaweza kuchukua siku kadhaa kufikia wagonjwa huku watoa huduma wakisafiri muda mrefu kwa barabara na hata kwa kutumia boti kwenye mito ili kufikisha huduma eneo husika.”

Picha ya WHO/Oka
Sampuli za damu zinachunguzwa katika maabara maalum mjini Mbandaka, katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

Mkurugenzi wa WHO kanda ya Afrika, Dkt. Matshidiso Moeti amesema kuwa “kukiwa tayari na wagonjwa 100 wa Ebola katika kipindi cha chini ya siku 100, mlipuko wa Ebola Equateur unasambaa kwa njia inayotia hofu. Virusi vinasambaa katika eneo pana na kuhitaji hatua zenye gharama kubwa na huku COVID-19 ikitumia rasilimali nyingi kuna changamoto kubwa kuimarisha operesheni zetu.”

Hatua za kudhibiti Ebola hivi sasa DRC hazijapata fedha zinazotakiwa na hivyo kuwa changamoto juu ya changamoto.
WHO ilikuwa ilitoa awali dola milioni 1.7 na kuongeza dola 600,000 kutoka mfuko wake wa dharura huku serikali ya DRC ikiwa imewasilisha ombi lake kwa wahisani la dola milioni 40 na yenyewe ikitenga dola milioni 4.

Dkt. Moeti amesema bila usaidizi wa ziada, timu zilizoko Equateur kukabiliana na Ebola zitakumbwa na wakati mgumu kudhibiti virusi vya Ebola. “COVID-19 si dharura pekee inayohitaji msaada wa kipekee. Kama tunavyofahamu sote kutokana na uzoefu wetu, kupuuza Ebola ni tishio kwetu wenyewe,” amesema Dkt. Moeti.

Hivi sasa kuna wataalamu 90 wa WHO huko Equateur na wengine 20 kutoka mashirika ya kimataifa.
Tangu kuanza kwa mlipuko huo wa 11, WHO imesaidia kampeni ya chanjo dhidi ya Ebola kwa zaidi ya watu 22,600 walioko hatarini kupata Ebola.

Mlipuko wa Ebola uliwahi kutoka jimboni Equateur mwezi Mei mwaka 2018 na ulidhibitiwa ndani ya miezi isiyozidi 3, ambapo kati ya wagonjwa 53 waliothibitishwa, 33 walifariki dunia.
 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud