Chonde chonde DRC chunguzeni vitisho vya mauaji dhidi ya Dkt. Mukwege- Bachelet 

28 Agosti 2020

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Michelle Bachelet ameeleza wasiwasi wake juu ya vitisho vya hivi karibuni vya mauaji dhidi ya mtetezi wa haki za binadamu nchini Jamhuri ya Kidemorkasia ya Congo, DRC na mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel, Dkt. Dennis Mukwege.

 

Msemaji wa Ofisi ya Haki za za binadamu ya Umoja wa Mataifa, Rupert Colville, akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi hii leo amemnukuu Bi Bachelet akisema kuwa, “nataka hatua za haraka za uchunguzi zifanyike ili kutambua ni nani anahusika na vitisho hivyo na afikishwe mbele ya sheria.” 

Dkt. Mukwege, ambaye ni muasisi na mwendeshaji wa hospitali ya Panzi kwenye mji wa Bukavu jimboni Kivu Kusini, alitambuliwa kimataifa ikiwemo tuzo ya amani ya Nobel ya mwak a2018 kwa kazi yake ya miongo kadhaa ya kusaidia kuwatibu maelfu ya wanawake waliokumbwa na ukatili wa kingono, hususan ubakaji na pia amekuwa mchehemuzi  dhidi ya wale wanoatumia ubakaji kama silaha ya vita akitaka pia ulinzi zaidi kwa wanawake. 

Bwana Rupert amesema kuwa Dkt. Mukwege pia “amekuwa kila mara akipaza sauti akitak awale wanaohusika na ukatili wa kingono wafikishwe mbele ya sheria na alikuwa mstari wa mbele kutetea ripoti yam waka 2010 ya ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa iliyoelezea mamia ya matukio ya ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu nchini DRC kati ya mwaka 1993 na 2003, ripoti iliyobainisha makundi yanayosadikiwa kuhusika na uhalifu huo wa kingono.” 

Kwa mujibu wa ofisi hiyo, Dkt. Mukwege amepata vitisho kadhaa vya kuuawa na alinusurika jaribio la kuuawa mwezi Oktoba mwaka 2012. 

“Ongezeko la vitisho vya mauaji hivi karibuni vilivyoenezwa kupitia mitandao ya kijamii na simu za moja kwa moja kwake na familia yake linafuatia hatua yake ya kulaani mauaji ya hivi karibuni ya raia mashariki mwa DRC na wito wake wa kutaka uwajibishwaji wa wale wanaokiuka haki za binadamu na wanaofanya ukatili,” amesema Bwana Colville. 

Bi. Bachelet amenukuliwa akisema kuwa maisha ya Dkt. Mukwege yako hatarini, “naunga mkono azma dhahiri ya Rais Etienne Tshisekedi wa DRC ya kuhakikisha usalama wake na natumai Dkt. Mukwege na timu yake watapatiwa ulinzi wa kutosha ili wawe na uhakika wa kuendelea kufanya kazi yao muhimu katika hospitali ya Panzi.” 

Halikadhalika ametaka uchunguzi wa haraka na huru wa vitisho dhidi ya Dkt Mukwege na wahusika wafikishwe mbele ya haki na ukweli ufahamike. 

 

 

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud