Bachelet yupo Ituri DRC kujadili ghasia za kikabila

23 Januari 2020

Kamishna Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet amewasili Bunia, mji mkuu wa jimbo la Ituri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC leo asubuhi kwa saa za huko na kuwa na mazungumzo na Waziri wa Mambo ya haki za binadamu na wajumbe wa kamati ya usalama wa jimbo hilo ambalo hivi hivi karibuni limekuwa limegubikwa na changamoto za kiusalama kutokana na mapigano ya kati ya wahema na walendu.

Kaimu gavana wa jimbo hilo Ibrahim Ucircan Bule amemweleza kamishna huyo kuwa wakati mwingine hali ya usalama imekuwa ni chanzo cha ukiukwaji mkubwa wa  haki za binadamu lakini amemshukuru Bi. Bachelet kwa usaidizi wake tangu kuanza kwa janga la ukiukwaji wa haki kwenye jimbo hilo hususan mji wa Djugu tangu mwaka 2017.

Kwa mujibu wa Bwana Bule, vitendo hivyo vya ukiukwaji wa  haki za binadamu vinatekelezwa na kikundi kilichojihami cha Codeco na kusisitiza kuwa juhudi zinafanywa na serikali ya DRC ili kutokomeza ghasia na kwamba kwa upande wa haki, watu kadhaa walikamatwa na kushtakiwa na mahakama ya kijeshi.

Hata hivyo amesema bado kuna changamoto na kumsihi mgeni wake asaidie juhudi za serikali kuu na ile ya jimbo hususan zile za mahakama.

Kwa upande wake, Waziri wa Haki za Binadamu, André Lite, ameongeza kuwa DRC ni mwanachama wa Umoja wa Mataifa na inahitaji msaada wa jamii ya kimataifa.

Akiwa Ituri Kamishna Mkuu Bachelet anakutana pia na wawakilishi wa makabila ya walendu na wahema ambapo watazungumzia ripoti ya vurugu za kikabila huko Djugu.

 

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter