Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ghasia zaripotiwa kwenye kampeni za uchaguzi DRC, UN yapaza sauti

Mabango ya kampeni za uchaguzi DRC
MONUSCO/M. Asmani
Mabango ya kampeni za uchaguzi DRC

Ghasia zaripotiwa kwenye kampeni za uchaguzi DRC, UN yapaza sauti

Haki za binadamu

 Ikiwa zimebakia siku 9 kabla ya kufanyika kwa  uchaguzi mkuu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, Kamishna Mkuu wa  haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa, Michelle Bachelet ameelezea wasiwasi wake mkubwa juu ya ghasia zilizoripotiwa katika majimbo matatu nchinu humo wiki hii wakati wa kampeni za uchaguzi.

Matukio hayo ni pamoja na lile la jimbo la Haut-Katanga ambapo watu wapatao watatu waliuawa na wengine kadhaa walijeruhiwa baada ya polisi kufyatua risasi na kutumia mabomu ya kutoa machozi dhidi ya waandamanaji wa wafuasi wa mgombea wa kiti cha urais Martin Fayulu, ambaye pia yaripotiwa alishambuliwa na polisi.

Halikadhilika akiwa Kalemie, jimbo la Tanganyika, kampeni ya Fayulu  ilikumbwa na tafrani na mtu mmoja aliuawa na wengine 9 walijeruhiwa.

Tukio la tatu ni huko Mbuji Mayi kwenye jimbo la Kasai Orientale ambapo gavana alituma askari na polisi kuzuia wtu wasisalimiane na mgombea wa uraisi kupitia upinzani, Etienne Tshisekedi ambapo mtoto mmoja mwenye  umri wa miaka 16 aliuawa na askari wa jeshi la DRC.

Pamona kutiwa wasiwasi na matumizi ya silaha za moto, Bi.  Bachelet ana wasiwasi pia na kitendo cha viongozi wa siasa kutumia kauli za kichochezi.

 Akimnukuu Bi. Bachelet, msemaji wa ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, Ravina Shamdasani amesema, “siku chache kabla ya uchaguzi muhimu DRC, ni muhimu mamlaka zihakikishe kuwa haki na uhuru wa kujieleza na kukusaninyika kwa amani zinalindwa na kwamba wanachukua hatua zote kuepusha ghasia. Hii inajumuisha kuhakikisha wagombea wote wanaweza kufanya mikutano na kampeni zao za uchaguzi.”

Kamishna Mkuu mpya wa haki za binadamu wa Umoja wa  Mataifa Michelle Bachelet akihutubia kikao cha Baraza la Haki za Binadamu la umoja huo huko Geneva, Uswisi
UN Photo - Jean-Marc Ferre
Kamishna Mkuu mpya wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet akihutubia kikao cha Baraza la Haki za Binadamu la umoja huo huko Geneva, Uswisi

Ofisi hiyo imesema kuwa wafuasi wa wagombea wa upinzani nao wameripotiwa kufanya ghasia kwenye mikutano ya kampeni ya mgombea wa chama tawala huko Kiwilu jimbo la Kasai.

“Katika mazingira ya uchaguzi ambayo tayari yana mvutano, naisihi serikali itumie ujumbe dhahiri kabisa kuwa vitisho na ghasia dhidi ya wapinzani wa kisiasa havitavumiliwa,” amesema Shamdasani akimnukuu Bi. Bachelet huku akiongeza kuwa, “naisihi serikali ya DRC ihakikishe vitendo kama hivyo vinachunguzwa  haraka na wahusika wawajibishwe.”

Ametoa wito pia kwa pande zote kujizuia kufanya ghasia na kusihi vikosi vya usalama visiegemee upande wowote.

Uchaguzi mkuu nchini DRC  unatarajiwa kufanyika tarehe 23  mwezi huu wa Desemba.

 

Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa, tafadhali jisajili na pia unaweza kupakua apu ili kuweza kusikiliza wakati wowote popote ulipo.