Kamishina mkuu wa haki za binadamu kuzuru DRC wiki hii

21 Januari 2020

Kamishna Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet Alhamisi wiki hii ataanza ziara ya siku tano nchini Jamhuri ya Kidemokarsia ya Congo, DRC kwa mwaliko maalum wa serikali.

Kamishina Mkuu atawasili Alhamisi Januari 23 Bunia katika jimbo la Kaskazini Mashariki mwa DRC la Ituri .

Akiwa Bunia Kamishina mkuu atatembelea kambi inayohifadhi wakimbizi wa ndani waliotawanywa na machafuko yanayoendelea baina ya Walendu na Wahema  na pia kufanya majadiliano na wawakilishi wa makundi yote mawili.

Pia atakutana na maafisa wa serikali wa eneo hilo, waathirika wa utesaji na wa ukatili wa kingono.

Tarehe 24 Januari Bi Bachelet ataelekea mji mkuu Kishasa ambako atakuwa na majadiliano ya siku tatu ambayo yatahusisha pia mkutano na Rais Tshisekedimnamo Januari 27.

Watu wengine atakaokutana nao mjini Kinshasa ni mawaziri wa mambo ya nje, ulinzi na haki na katiba, lakini pia waziri wa haki za binadamu, watoto na familia pamoja na maafisa wengine wa serikali.

Bi. Bachelet pia atakuwa na majadiliano na tume ya kitaifa ya haki za binadamu, mashirika ya asasi za kiraia, wakuu wa mashirika ya Umoja wa Mataifa DRC, maafisa wengine wa mpango wa Umoja wa Mataifa nchini humo MONUSCO na mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu DRC Bi. Leila Zerrougui.

Na mwisho wa ziara yake hapo Januari 27 Bi Bachelet atatoa taarifa kuhusu ziara hiyo.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter