Ni wajibu wangu kuwasaidia na kuwalinda watoto hata wakati wa COVID-19: Sreyoun

24 Agosti 2020

Kutana na mtaalam wa huduma za kijamii za watoto nchini Cambodia Tim Sreyoun ambaye anasema licha ya janga la corona au COVID-19 ni wajibu wake kuhakikisha watoto wanahudumiwa na kulindwa dhidi ya ukatili kwani ni zahma aliyoipitia maishani mwake.

Mjini Battambang nchini Cambodia huyo ni Tim Sreyoun mtaalam wa ustawi wa jamii ambaye kazi yake kubwa ni kuwalinda watoto dhidi ya ukatili na anafanya kazi na idara ya serikali ya ustawi wa jamii jimboni hapo.  

Kwa mujibu wa shirika la kuhudumia watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF ukatili dhidi ya watoto ni changamoto kubwa nchini Cambodia na janga la COVID -19 limefanya hali kuwa mbaya zaidi. Tim anasema “Tumekuwa tukitoa taarifa kuhusu COVID-19 na ukatili kwa familia na jamii na tunawasaidia watoto katika afya ya akili kwa sababu watoto wengi wameogopa sana kufuatia janga hili” 

UNICEF imefanya utafiti katika nchi 104 na zote zimearifu kuhusu kuathirika kwa huduma za ustawi wa jamii kwa watoto hasa za kupambana na ukatili ikiwemo Cambodia na mikakati ya kujikinga na corona imeongeza madhila kwa watoto hasa nchini Cambodia hali inayothibitishwa na Tim “Tangu kuzuka kwa janga la COVID-19 ukatili majumbani umeongezeka kwa kasi na hatuwezi kuwasaidia watoto haraka kwa sababu ya vikwazo vya kutembea, hatuwezi kuwafuata mashinani waliko. Lakini ninahitaji kutimiza wajibu wangu huku nikizingatia masharti ya kutochangamana. Hivyo badala yake sasa inanibidi niwapigie simu watu ninaowahudumia” 

Tim ambaye binafsi alipitia ukatili majumbani hata ukamsukuma kuingia katika kazi hiyo ya kusaidia watoto walioathirika ameahidi hata iweje ni lazima atimize wajibu wake. “Sasa mimi ni mtu ambaye nina jukumu muhimu la kuwasaidia watoto hawa wanaopitia ukatili, hivyo asilani katika mazingira yoyote yale sintowaacha nyuma” 

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter