Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kila msumari utumikao kwenye ujenzi ni kiashiria cha kufunika jeneza la ukatili dhidi ya mtoto Sudan Kusini- UNMISS

Watoto wakicheza katika kambi vitongoji vya Aweli, kasakzini mwa Bahr el-Ghazal, kaskazini mwa Sudan Kusini
Picha: IRIN/Siegfried Modola
Watoto wakicheza katika kambi vitongoji vya Aweli, kasakzini mwa Bahr el-Ghazal, kaskazini mwa Sudan Kusini

Kila msumari utumikao kwenye ujenzi ni kiashiria cha kufunika jeneza la ukatili dhidi ya mtoto Sudan Kusini- UNMISS

Haki za binadamu

Jeshi nchini Sudan Kusini, SSPDF, limechukua hatua madhubuti kuhakikisha ulinzi wa mtoto kwa kujenga ofisi maalum la ulinzi wa watoto ambao kila uchao hukumbwa na madhila ikiwemo ukatili wa kingono na utumikishwaji jeshini.

Ujenzi wa kituo hicho unafanyika kwenye makao makuu ya jeshi la Sudan Kusini yaliyopo mji mkuu Juba, kwa ufadhili wa  ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, UNMISS.

Wajenzi wanaendelea na kazi ya  ujenzi wa msingi na ukuta madhubuti wa jengo hilo na vifaa vyote vipo kwenye eneo la ujenzi ikiashiria kuwa utakamilika kwa wakati.

Jengo litakuwa na ofisi nne, chumba cha mkutano, eneo la mapokezi na ushoroba.

Maafisa waandamizi wa jeshi wamekuwa wakifuatilia ujenzi kama anavyoelezea Meja Jenerali Chaplain Khamis Edward, Mkuu wa kitengo cha ulinzi wa mtoto kwenye jeshi la Sudan Kusini ambaye amesema,  “katika ulinzi wa mtoto tunatatua mambo sita ambayo hatutaki yaendelee ndani ya jeshi na nje ya jeshi. Tunataka kutokomeza matumizi na utumikishaji watoto jeshini. Ukaliaji wa shule, utekaji watoto, ukatili wa kingono dhidi ya watoto, kuzuia ufikishaji wa huduma. Watoa huduma wasambaze huduma watakako na tutakuwa nao pamoja.”

Mtoto wa kike akiwa amesimama nje ya makazi ya muda ya kulinda raia huko Bentiu nchini Sudan Kusini.
UNICEF/Holt (file)
Mtoto wa kike akiwa amesimama nje ya makazi ya muda ya kulinda raia huko Bentiu nchini Sudan Kusini.

Ufadhil wa ujenzi huu ni chini ya mradi wa matokeo ya haraka, QIP wa UNMISS ambao huleta kuboresha maisha  ya jamii Sudan Kusini kote na Mkuu wa kitengo cha ulinzi wa mtoto, U NMISS Alfred Orono-Orono anafafanua ya kwamba, “kila tofali hapa linaashiria aina ya umoja kati yetu na jeshi la Sudan Kusini, SSPDF, na kila msumari unaotumika hapa ni msumari wa jeneza la kifo cha masuala ya ukiukwaji wa haki za mtoto Sudan Kusini. Hili ni jengo muhimu sana kwetu sisi.”

Matumaini ni kwamba kukamilika kwa jengo hili ni fursa sasa ya kuanza hatua za dhati za ulinzi wa mtoto Sudan Kusini dhidi ya vitendo vya ukatili vinavyofanywa na makundi yaliyojihami kwenye taifa hilo changa zaidi duniani.

Bwana Orono-Orono amesema ofisi hiyo itakuwa na afisa kutoka UNMISS na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF, ambaye atawajengea uwezo maafisa wa jeshi la Sudan Kusini kuhakiksha kuwa suala la ulinzi wa mtoto linachipua na kuwa sehemu ya vikosi vya usalama Sudan Kusini.”

Awali masuala ya ulinzi wa mtoto yalikuwa yakishughulikiwa kwenye jengo chakavu lililojengwa mwaka 2009.