COVID-19 imeingilia na kuathiri huduma za ulinzi wa watoto katika nchi zaidi ya 100: UNICEF

Mfanyikazi wa jamii (kushoto) na mwanasaikolojia (wa pili kutoka kushoto) wakipeana vitabu vya kuchorea kwa watoto mashariki mwa Ukraine, wakati wa ziara ya nyumbani.
© UNICEF/Zmey
Mfanyikazi wa jamii (kushoto) na mwanasaikolojia (wa pili kutoka kushoto) wakipeana vitabu vya kuchorea kwa watoto mashariki mwa Ukraine, wakati wa ziara ya nyumbani.

COVID-19 imeingilia na kuathiri huduma za ulinzi wa watoto katika nchi zaidi ya 100: UNICEF

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Huduma za kupambana na ukatili na ulinzi kwa watoto zimeathirika vibaya wakati huu wa janga la corona au COVID-19 na kuwaacha watoto katika hatari kubwa ya machafuko, unyanyasaji na ukatili kwa mujibu wa utafiti wa kimataifa uliofanywa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF.

UNICEF inasema matokeo ya utafiti huo yaliyotokana na maoni yaliyokusanywa kutoka nchi 104 kati ya nchi 136 kuhusu athari ya kiuchumi na kijamii za COVID-19 yameonyesha kwamba kumekuwa na athari za uingiliaji wa huduma muhimu zinazohusu kuzuia ukatili dhidi ya watoto. 

Utafiti huo unasema takriban theluthi mbili ya nchi zimeripoti kwamba angalau huduma moja imeathirika vibaya ikiwemo Afrika Kusini, Malaysia, Nigeria na Pakistan na nchi za Kusini mwa Asia, Ulaya Mashariki na Asia ya Kati ndizo zilizoripoti kiwango kikubwa cha kuathirika kwa huduma hizo. Hlin ni mfanyakazi wa huduma za jamii katika mji mkuu wa Iceland, Reykavijik ukumu lake kubwa likiwa ni kulinda watoto waliopitia unyanyasaji au ukatili anasema "Tulichokishuhudia ni kwamba kumekuwa na ongezeko kubwa kwa mfano la ukatili majumbani ambao watoto walio majumbani wanaushuhudia. Tumepokea ripoti za matumizi mabaya ya pombe na madawa majumbani na kwa ujumla watoto wameripoti kutojihisi salama” 

Kwa upande wake mkurugenzi mkuu wa UNICEF Henrieta Fore amesema “sasa ndio tunaanza kuelewa kwa kina athari zinazowasibu watoto kwa kushuhudia ongezeko la machafuko wakati wa hatua za kusalia majumbani kukabiliana na COVID-19. Kuendelea kufungwa kwa shule na vikwazo vya kutembea vimewafanya baadhi ya watoto kukwama majumbani na wakatili wao. Athari za huduma za ulinzi na kwa wafanyakazi wa huduma za jamii inamaanisha kwamba watoto hawana popote pa kupata msaada.” 

Utafiti huo pia umesema hata kabla ya janga la COVID-19 watoto walikuwa tayari wanashuhudia ukatili katika sehemu mbalimbali duniani huku karibu nusu ya watoto wote duniani wakipitia adhabu majumbani, takribani watatu kati ya wane wa umri wa miaka 2 hadi 4 wakipewa adhabu za aina fulani na wasichana vigori mmoja kati ya watatu wa umri wa miaka 15 hadi 19 wakipitia ukatili kutoka kwa wapenzi wao .

Ili kukabiliana na hali hiyo UNICEF inazisaidia serikali na mashirika wadau kuhakikisha zinachukua hatua madhubuti za ulinzi na huduma kwa watoto walioathirika na ukatili wakati wa COVID-19 katika nchi mbalimbali ikisema kwamba “watoto wengi wanategemea mfumo wa ulinzi kwa Watoto ili kuwahakikishia usalama wao.”