Ukiukwaji wa haki Sudan Kusini wakwamisha mkataba wa amani- Kamisheni

Watoto Sudan Kusini
UNMISS/Ilya Medvedev
Watoto Sudan Kusini

Ukiukwaji wa haki Sudan Kusini wakwamisha mkataba wa amani- Kamisheni

Haki za binadamu

Kamisheni ya haki za binadamu kwa Sudan Kusini imeeleza wasiwasi wake mkubwa juu ya kuendelea kwa ghasia hivi karibuni katika majimbo 6 kati ya 10 nchini humo.

Taarifa ya kamisheni hiyo iliyotolewa leo mjini Juba, Sudan Kusini na Geneva, Uswisi inataja majimbo hayo kuwa ni Equatoria ya Kati, Jonglei, Lakes, Unity, Bahr el-Ghazal Magharibi na Warrap, mapigano ambayo yamesababisha vifo na majeruhi miongoni mwa raia huku watu wengine zaidi ya 80,000 wakisalia wakimbizi wa ndani.

Aina za ukatili

“Ukatili na uharibifu uliofuatia mapigano hayo umesababisha mamia ya wanawake na watoto kutekwa nyara, wanawake na watoto wa kike hata wenye umri wa miaka 8 kubakwa au kukumbwa na aina mbali mbali za ukatili wa kingono na ukatili wa kijinsia,” imefafanua taarifa hiyo.
 
Ikifafanua zaidi, ripoti hiyo imesema katika majimbo ya Jonglei na Warrap, ghasia imechochewa na mapigano ya kikabila na mauaji ya kulipiza kisasi, “mashambulizi mengi yamehusisha vikosi vya jeshi la serikali, SSPDF, na wafuasi wa vikundi vya upinzani vilivyojihami.”

Katika tukio la hivi karibuni zaidi la tarehe 8 mwezi huu wa Agosti, watu 75 waliuawa na wengine 76 walijeruhiwa kufuatia mapigano makali kati ya vijana waliojihami wa kabila la wadinka na askari wa SSPDF walioko jimboni Warrap.

Taarifa inasema kuna matukio ya ubakaji wanawake kwa magenge huko jimboni Warrap na Lakes.

Mtu mwenye silaha katika mji wa Pibor, jimbo la Jonglei Sudan Kusini. Pibor umeshudia makabiliano yaliyosababisha watu kuhama na makazi yao kuharibiwa.
(Picha maktaba) OCHA/Cecilia Attefors
Mtu mwenye silaha katika mji wa Pibor, jimbo la Jonglei Sudan Kusini. Pibor umeshudia makabiliano yaliyosababisha watu kuhama na makazi yao kuharibiwa.

Mwenyekiti wa Kamisheni hiyo Yasmin Yooka anasema kuwa, “kiwango cha ghasia na machungu ambayo wanawake, wazee na watoto wanakumbana nayo kwenye majimbo hayo kinachukiza na kinaonesha ni kwa kiwango gani utu wa mtu unapuuzwa na kugeuza mkataba wa amani Sudan Kusini kuwa ni kituko.”

Ghasia na utapiamlo

Pamoja na ghasia kuchochea ukatili wa kijinsia na kingono, Bi. Sooka amesma pia imesababisha ongezeko la unyafuzi miongoni mwa watoto wachanga na watoto akisema kuwa, “hali hii inatokea wakati idadi kubwa ya raia hususan wakimbizi milioni 1.6 wa ndani wanaendelea kuwa hatarini kukumbwa na ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19 na hawana huduma za kutosha za msingi kama vile maji safi na huduma za kujisafi.”

Kamisheni hiyo imesalia na hofi kubwa kuwa pande kinzani Sudan Kusini zimepuuza wito wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa aliotoa tarehe 23 mwezi Machi mwaka huu kwa pande kinzani katika mizozo kusitisha mapigano ili kuelekeza nguvu zao kwenye kukabiliana na COVID-19.

Wajumbe wa kamisheni hiyo wamesema pamoja na kukaribisha taarifa ya Rais Salva Kiir ya kuongeza juhudi za kutekeleza mkataba wa amani, bado kuna hofu kuwa wahusika wa matukio ya karibuni ya ukatili watawajibishwa.

Mmoja wa makamishna wa tume hiyo, Barney Afako ameonya kuwa, “kuchelewa kutekelezwa kwa mkataba mpya kunatishia ombwe la uongozi katika ngazi ya majimbo na kati, hali inayoweza kusababisha kuongezeka kwa ghasia ambazo zinashuhudiwa hivi sasa Sudan Kusini.”

Mlinzi wa kikosi cha kulinda amani Sudan Kusini kutoka China akiwa anashika doria mjini Juba.Picha
UNMISS(Picha ya Maktaba July 2018)
Mlinzi wa kikosi cha kulinda amani Sudan Kusini kutoka China akiwa anashika doria mjini Juba.Picha

Serikali inachelewesha mkataba wa amani

Kamisheni hiyo imesema licha ya kuundwa kwa serikali mpya tarehe 22 mwezi Februari mwaka huu wa 2020 kwa mujibu wa mkataba mpya wa amani, bado utekelezaji wa mkataba unasuasua.

Mathalani kuundwa kwa Bunge jipya la mpito, jambo linalotowesha matumaini ya kupitishwa kwa sheria za kuanzishwa kwa Tume ya Ukweli na Maridhiano na Mahakama Kuu ya Sudan Kusini na mamlaka ya ulipaji fidia.

Kamisheni hiyo imetoa wito kwa serikali kutekeleza vipengele vya mkataba mpya ili kuziba ombwe hilo na kutaka pande zote kusitisha mapigano.

Kamisheni ya Haki za Binadamu kwa Sudan Kusini ilianzishwa na Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa mwezi Machi mwaka 2016 na kuongezewa muda hadi Machi 2017 na kisha 2018, 2019 na Juni 2020 na kupatiwa mamlaka ya kubaini ,kukusanya taarifa na kuripoti ushahidi wa ukiukwaji wa haki za binadamu kwa lengo la kutokomeza ukwepaji haki.