Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tuwawezeshe vijana duniani kote ili wachangie katika hatua za pamoja za kimataifa-Guterres

Vijana wakiandamana kupigania usawa wa kijinsia na haki za wanawake huko Nepal.
UN Women/Uma Bista
Vijana wakiandamana kupigania usawa wa kijinsia na haki za wanawake huko Nepal.

Tuwawezeshe vijana duniani kote ili wachangie katika hatua za pamoja za kimataifa-Guterres

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Ikiwa leo ni siku ya kimataifa ya vijana, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres kupitia ujumbe wake kuhusu siku hii inayolenga ushiriki wa vijana katika hatua za pamoja za kimataifa, ametoa wito kwa viongozi na watu wazima kote duniani kufanya kila linalowezekana kuwawezesha vijana wa ulimwengu kufurahia maisha ya usalama, utu pia fursa na kuchangia katika hatua za pamoja za kimataifa.  

Katibu Mkuu Guterres amesema siku ya vijana ya mwaka huu inatokea wakati maisha na matarajio ya vijana yanaendelea kuvurugwa na janga la COVID-19 na baadhi yao wamepoteza maisha, na wengine wamewaona wanafamilia wao na wapendwa wao wengine wakipoteza maisha na kwamba hali ya hatari kwa wakimbizi vijana, watu waliotawanywa, wasichana na wengine ambao wamekwama katika mzozo wamepatikana kwenye mzozo au janga imekuwa kubwa zaidi.  

“Malezi ya kizazi yamehatarishwa, hatua zao kuelekea utu uzima, utambulisho na kujitosheleza, vimetupwa mbali. Wengine wamechukua mizigo ya kulea au wanateswa na hatari zinazoongezeka za njaa, unaynyasaji majumbani au matarajio ya kutoweza kuendelea tena na masomo. Lakini kizazi hiki pia ni chenye mnepo, nguvu na kinashiriki. Ni vijana ambao wameamka kudai hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi. Wanahamasisha haki ya usawa na haki ya rangi zote na usawa wa kijinsia na ni wasongezaji wa ulimwengu endelevu zaidi." 

Aidha Katibu Mkuu Guterres amesema wengi ni wanawake vijana ambao wamekuwa mstari wa mbele katika uhamasiushaji wa haki na hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na pia wakihudumu kwenye mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya COVID-19 na kwa hivyo kutambua ahadi ya kizazi hiki kunamaanisha kuwekeza zaidi katika ujumuishaji wa vijana, ushiriki, mipango na mikakati. “Ninatoa wito kwa viongozi na watu wazima popote, kufanya kila linalowezekana kuwawezesha vijana wa ulimwengu kufurahia maisha ya usalama na fursa ili kuchangia kwa uwezo wao wote.”