Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Leo tunawasherehekea wafanyao kazi kubadili elimu na kuwainua vijana kila mahali-Antonio Guterres

Picha ya maktaba ikiwaonesha vijana baadhi walipokuwa katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa kuadhimisha siku ya kimataifa ya vijana
UN Photo/Kim Haughton
Picha ya maktaba ikiwaonesha vijana baadhi walipokuwa katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa kuadhimisha siku ya kimataifa ya vijana

Leo tunawasherehekea wafanyao kazi kubadili elimu na kuwainua vijana kila mahali-Antonio Guterres

Masuala ya UM

Katika kuiadhimisha siku ya kimataifa ya vijana, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameweka msisitizo zaidi katika mada ya  mwaka huu ya kufanya mabadiliko katika elimu ili kuifanya kuwa jumuishi zaidi, rahisi kupatikana na inayokwenda na dunia ya sasa. 

Ni Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa akianza kwa kueleza kuwa siku hii ya kimataifa ya vijana inaadhimishwa hivi sasa kwa mwaka wa 20. Bwana Guterres kupitia ujumbe wake huu anasema,

(Sauti ya Guterres)

“tunakabiliwa na mgogoro wa kujifunza, mara nyingi shule haziwapatii vijana ujuzi wanaohitaji kwenda sanjari na mapinduzi ya teknolojia. Wanafunzi wanachohitaji si kusoma tu bali pia kusoma jinsi ya kujifunza.”

Aidha Bwana Guterres ameendelea kueleza kuwa elimu ya sasa inapaswa kujumisha ufahamu, stadi za maisha na fikira za uchambuzi. Inapaswa kujumuisha taarifa kuhusu uendelevu na mabadiliko ya tabia nchi, usawa wa jinsia, haki za binadamu na utamaduni wa amani. Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa ameongeza kusema kuwa vitu vyote hivyo viko katika ajenda ya vijana ya mwaka 2030, mkakati wa Umoja wa Mataifa wa kuongeza ushirikishaji wa vijana katika kufikia haki zao.

Katibu Mkuu Guterres anahitimisha ujumbe wake akisema,

(Sauti ya Guterres)

“Leo tunawasherehekea vijana, mashirika yanayoongozwa na vijana, serikali na wengineo wafanyao kazi kubadili elimu na kuwainua vijana kila mahali.”