Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mshikamano wa marika yote unawasaidia vijana kufikia malengo yao kwa haraka

Kijana anayejishughulisha na ufinyanzi mkoani Tabora Tanzania
UN News
Kijana anayejishughulisha na ufinyanzi mkoani Tabora Tanzania

Mshikamano wa marika yote unawasaidia vijana kufikia malengo yao kwa haraka

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Tarehe 12 mwezi Agosti kila mwaka ni siku ya vijana duniani, siku hii inakuja na ujumbe aina tofauti kila mwaka na mwaka huu vizazi vyote vinatakiwa kushirikiana na vijana ili kufanikisha kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu SDGs ifikapo mwaka 2030. 

Siku hii inaadhimishwa huku kukiwa na taarifa kuwa nusu ya wakazi wote duniani wana umri wa miaka 30 au chini ya hapo na idadi hii inatarajiwa kuwa asilimia 57 ifikapo mwishoni mwa mwaka 2030.

Pamoja na wingi wao kwenye sayari dunia, vijana wamekuwa wakieleza mara kwa mara kukabiliwa na vikwazo fulani vya mshikamano kati yao na marika mengine kwenye jamii na wamekuwa wakionekana hawakidhi vigezo kwenye maeneo kama ya ajira, afya, haki na nafasi za uongozi wa kisiasa na nafasi hizo kujazwa na wale wenye umri mkubwa zaidi yao. 

Lakini baadhi ya vijana wanaeleza kuwa pale wanaposhikwa mkono na wazee au wale walio na umri mkubwa wamekuwa wakipata mafanikio makubwa na kwa haraka. 

Happiness Palangyo kutoka Radio washirika Radio Uhai FM ya mkoani Tabora Tanzania amezungumza na vijana amoja na mkufunzi wa vijana ambao wote kwa nyakati tofauti wamekiri kuwa mshikamo wa marika yote unawasaidia Zaidi vijana kufikia malengo yao kwa wakati tofauti na kuwaacha wenyewe bila muongozo wowote. 

Akizungumza na binti Ezereda Mwahele amemueleza yeye mafaniko yake yalitokana na kupata muongozo madhubuti kutoka kwa wazee waliomzunguka.

“Wazee wamechangia kwa sehemu kubwa sana katika mafanikio yangu, jambo la kwanza nisingeweza kufika mahali hapa bila watu walionizidi umri, wameweza kunilea na kuniongoza na kunielekeza ili kukua katika maadili ambayo yananifanya kuwa kijana ninayjitambua lakini wazee wameweza kunishauri kupita njia ambazo naweza kuyafikia malengo na mafanikio ambayo nimejiwekea”

Kijana mwingine ni Jaylose Julius, yeye ni kijana mwenye ulemavu wa macho ambaye amejikita katika shughuli za ufinyanzi na anasema mafanikio yake yamechangiwa na ushauri aliopewa na wa watu waliomzidi umri.

“Wazee wamenisaidia vitu vingi sana na ninapozungumzia wazee, wazee wetu zamani ndio vitu ambavyo vinahusiana na kazi za mikono ambazo ni ufinyanzi baada ya kuingia kwenye fani hii kuna bibi mmoja mimi ndio alinifundisha kufinyanga hivi vitu kwa hiyo umuhimu wa wazee ni pamoja na yule mzee bibi ambaye alinifundisha mimi kwa kazi hii ya ufinyanzi kwa sababu amenitoa hatua moja kwenda hatua nyingine”.

Pia kijana huyu mwenye ulemavu wa macho anasema vijana wa aina yake wasikate tamaa ya kutokufanya kazi bali wajishughulishe na kazi yoyote iliyo ndani ya uwezo wao kwani ulemavu sio ugonjwa.

Ezereda Mwahele Kijana kutoka Tanzania
UN News
Ezereda Mwahele Kijana kutoka Tanzania

“Kwa upande wa vijana wengi wenye ulemavu hawapendi kujishughulisha kwa kazi yoyote ile ambayo kwao itawaingizia kipato ulemavu sio kigezo cha kusema uwezi kufanya kazi hapana bali ni sehemu ya kufanya kazi katika mazingira yoyote yale ili kupata kipato na kuacha utegemezi” 

Hapiness pia alifunga safari na kufanya mazungumzo na Mkuu wa chuo cha Comenius Polytechnic Institute Tabora nchini Tanzania Ezekiel Kasanga ambaye alisema vijana ili wafanikiwe katika maisha yao wanahitaji mwongozo, wanahitaji kushauriwa pamoja na kuwezeshwa.

“Tunawaanda vijana namna wanavyoingia kwenye mafanikio kupata ajira na kutengeneza ajira haya mambo iliyafanyike lazima wazee au watu wa umri wa kati wawasaidie vijana kwa sababu wanayonguvu,elimu na maarifa”