Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kutoka taka za plastiki baharini mpaka malighafi ya kutengenezea matofali

Taka ngumu za plastiki ikikokotwa kutoka majini ilipokuwa imetupwa na wavuvi wa ufukwe wa Mihama Jijini Mwanza Nchini Tanzania.
UN News/Evarist Mapesa
Taka ngumu za plastiki ikikokotwa kutoka majini ilipokuwa imetupwa na wavuvi wa ufukwe wa Mihama Jijini Mwanza Nchini Tanzania.

Kutoka taka za plastiki baharini mpaka malighafi ya kutengenezea matofali

Tabianchi na mazingira

Dunia inakabiliwa na mabadiliko ya tabia nchi na uchafuzi wa mazingira ambayo tayari yameanza kuleta athari hasi kwa binadamu, wanyama na viumbe hai waishio majini ikiwemo Samaki katika maeneo mbalimbali ulimwenguni.

Hata hivyo lengo namba 14 la Malengo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDGs) linazungumzia Maisha ya viumbe hai waishio chini ya maji na kusisitiza matumizi endelevu na uhifadhi wa rasilimali zilizopo baharini ifikapo mwaka 2030.

Umoja wa Mataifa umekuwa ukisisitiza nchi wanachama kuhakikisha wanadhibiti aina zote za uchafuzi ikiwa ni pamoja na taka za plastiki zinazotupwa maeneo ya Bahari, Ziwa na Mito ili kulinda mifumo ya ikolojia na kuepusha athari mbaya kwa viumbe hai.

Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP), Zaidi ya tani milioni 400 za plastiki huzalishwa kila mwaka kote duniani, nusu ya taka hizo hutumika tu mara moja, Kati ya hizo, chini ya asilimia 10 ya plastiki huchakatwa, na kila mwaka takriban tani kati ya milioni 19 na milioni 23 huelekea kwenye Maziwa, Mito na Bahari.

Ili kulinda maisha ya viumbe hai waishio chini ya maji, vijana Nchini Tanzania wameanzisha taasisi inayojulikana kwa jina la Arena Recycling inayo jihusisha na ukusanyaji wa taka hususani za plastiki zinazotupwa katika maeneo mbalimbali ya fukwe na kuzigeuza kuwa bidhaa.

Taasisi hiyo huzikusanya taka hizo kutoka katika fukwe za Ziwa Victoria, Nyasa, Tanganyika na bahari ya Hindi na kisha huzichakata tena plastiki hizo na kisha kutengeneza bidhaa mbalimbali kama matofali, na vigae.

Matofali yakiwa tayari yamezalishwa kutokana na taka za plastiki zilizorejelezwa na kisha kuchanganwa na kiasi fulani cha mchanga wa kutengenezea bidhaa hizo, mradi ulioanzishwa na vijana kutoka Mwanza Tanzania.
UN News/Evarist Mapesa
Matofali yakiwa tayari yamezalishwa kutokana na taka za plastiki zilizorejelezwa na kisha kuchanganwa na kiasi fulani cha mchanga wa kutengenezea bidhaa hizo, mradi ulioanzishwa na vijana kutoka Mwanza Tanzania.

Kwanini wanakukusanya taka za plastiki katika fukwe?

Uchafuzi huo wa mazingira ni mwiba mkali kwa viumbe hai waishio chini ya maji kutokana na taka ngumu kama plastiki kutiririshwa baharini, mitoni na maeneo ya ziwani hivyo kuendelea kuhatarisha Maisha ya Samaki ambao kwa sasa wapo hatarini kutoweka.

Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) katika ripoti yake ya mwaka 2022 ilieleza kuwa idadi ya uchafu wa plastiki inayoingia kwenye mifumo ya ekolojia ya majini imeongezeka kwa miaka ya hivi karibuni na inakadiriwa kuongezeka maradufu kufikia mwaka wa 2030.

Kwa mujibu wa mwanzilishi wa taasisi ya Arena Recycling Zagalo Emmanuel anasema wazo la kuanza kukusanya taka za plastiki lilianza miaka minne iliyopita, baada ya kutambua changamoto iliyopo katika miji inayoendelea.

“wazo nililipata nikiwa na wenzangu na kutambua changamoto iliyopo katika miji iliyoendelea kama Dar Es Salaam, inauzalishaji mkubwa wa taka hasa plastiki hivyo tukaona ni fursa kwetu.”

Wazo lilitokana na nini?

Kwa mujibu wa Zagalo, wazo la kuanzisha mradi huu alilipata akiwa chuoni kati yam waka 2018 na 2019 alipokutana na vijana wenzake na kugundua kuwa katika miji mikubwa hususani jiji la kibiashara la Dar es Salaam nchini Tanzania kuna uzalishaji mkubwa wa taka hasa za plastiki.

“Uzalishaji wa taka ni mkubwa katika miji iliyoendelea, hivyo tuliona ni fursa kwetu kuweza kuangalia jinsi gani tunaweza kubadili tatizo lile kuwa fursa”.

Zagalo ameongeza kuwa “Wakati huo huo tuliona katika miji iliyoendelea kuna uhaba wa makazi na watu wengi katika maeneo hayo wanaishi kwa kupanga kutokana na kutokuwa na uwezo wa kujenga nyumba kwa sababu ya gharama kubwa za ujenzi kama theluji na tofali”.

Na kutokana na changamoto hiyo vijana hao wakaona ni fursa kwao ya kuuwa ndege wawili kwa jiwe moja.

Zagalo Emmanuel ,Mwanzilishi wa Mradi kukusanya taka za plastiki na kuzibadilisha kuwa bidhaa za ujenzi nchini Tanzania.
UN News/Evarist Mapesa

“Tuliamua kuja na ubunifu huu uliweza kusaidia kutatua tatizo la ongezeko la taka za plastiki na pia kutengeneza bidhaa za ujenzi ambazo mwananchi anauwezo wa kuzimudu. Tunatengeneza tofali za plastiki ambazo hazitumii theluji wala maji na kama zikitumia hivyo vitu basi ni kwa kiasi kidogo sana, hivyo inapunguza gharama za ujenzi kwa kiasi kikubwa”, alisema Zagalo.

Kutokana na kazi hiyo ya kukusanya taka za plastiki na kuzibadilisha matumizi yake, wanajivunia tofali wanazozizalisha kutokana na uimara wake unaoweza kudumu kwa kipindi kirefu.

“Tofali zetu ni mara mbili ya tofali za kawaida, zinaweza kudumu kwa miaka mingi Zaidi kama unavyojua plastiki inadumu kwa miaka mingi hivyo mchanganyiko wa plastiki na mchanga, unadumu Zaidi”, alisema Zagalo.

Wanazibadilishaje plastiki hizo kuwa bidhaa?

Ili kuweza kubadilisha matumizi ya kitu chochote cha kisayansi huhitaji mashine ama vifaa vitakavyosaidia mchakato huo kukamilika.

Zagalo anasema wamekuwa wakitumia teknolojia ya kawaida, licha ya mashine zenye uwezo wa kufanya hivyo huwa na gharama kwa kiasi fulani lakini waliweza kumudu kwa kuanza na mtaji wao binafsi na kisha walianza kupata ufadhili kutoka Shirika la Msaada wa watu wa Marekani (USAID) Pamoja na Young Water Solution, ambazo ziliwasaidia kununua vifaa vingine.

“Kwanza kabisa huwa tunakusanya taka za plastiki, kisha tunazikata kuwa vipande vidogo, baada ya hapo kama lengo letu ni kutengeneza tofali huwa tunachanganya na mchanga, tukisha changanya na mchanga basi tunayeyusha mchanyanyiko huo na kuuweka katika umbo la tofali ambalo unataka kulitengeneza”.

Unapoliyeyusha linakuwa katika mfumo wa uji uji ambao umechanganyikana na mchanga, baada ya kukauka au kupoa unakuwa umetengeneza bidhaa ambayo ni mara dufu ya tofali la kawaida kwakua lina uwezo wa kuishi miaka 50 mpaka 60”, alisema Zagalo.

Kutokana nah atua hizo za ubadilishaji wa taka za plastiki wamefanikiwa kujenga vyumba vya vyoo katika shule za msingi za Karume na Buza zilizopo katika Wilaya ya Temeke Jijini Dar Es Salaam nchini Tanzania ambazo matofali yake yalitokana na taka za Plastiki.

Wanawake na vijana nchini Tanzania wakikusanya taka za plastiki ambazo zitakarabatiwa na kubadilishwa kuwa vifaa vya ujenzi kama vile Matofali.
UN News/Evarist Mapesa
Wanawake na vijana nchini Tanzania wakikusanya taka za plastiki ambazo zitakarabatiwa na kubadilishwa kuwa vifaa vya ujenzi kama vile Matofali.

Upatikanaji wa plastiki nchini Tanzania upoje?

June Mosi, 2019 Tanzania iliungana na mataifa mengine ya Afrika Mashariki kama Rwanda, na Kenya kupiga marufuku matumizi na uzalishaji wa mifuko ya plastiki katika kutekeleza makubaliano ya kimataifa ya kulinda mazingira dhidi ya bidhaa za plastiki.

Marufuku hiyo iliyotolewa na Serikali ya Tanzania ilibainisha kuwa ni kosa kwa mtu yeyote kutengeneza, kuingiza, kusambaza na kutumia mifuko ya Plastiki lengo ikiwa nikutokomeza kueneo kwa taka inayotokana na mifuko hiyo kwenye mazingira.

Kwa mujibu wa serikali ya Tanzania katika maelezo yake waliyoyatoa Mei 31, 2019 ikiwa ni siku moja kabla ya marufuku waliyoitoa, ilieleza kuwa taka za plastiki zinaharibu udongo, huzalisha gesi za sumu, huleta madhara ya kiafya kwa binadamu na Wanyama Pamoja na kutooza kirahisi.

Licha ya marufuku hiyo lakini bado taka za plastiki zimekuwa zikionekana kwa wingi katika maeneo ya kutupa uchafu kutokana na baadhi ya bidhaa kama sabuni, nguo, sukari, unga, na chumvii kufungashiwa katika mifuko ya plastiki.

Kwanini Taka za Plastiki ni hatari kwa viumbe hai?

Ripoti ya UNEP ya mwaka 2021 inaonesha kwamba plastiki huchangia asilimia 85 ya takataka za baharini na inaonya kuwa kufikia mwaka wa 2040, kiwango cha uchafu wa plastiki katika maeneo ya baharini kitaongezeka karibu mara tatu.

Hata hivyo Umoja wa mataifa mara kadhaa umekuwa ikionya kuwa iwapo mataifa hayatochukua hatua za mapema kudhibiti taka zitokanazo na plastiki, huenda ulimwengu ukashuhudia idadi kubwa ya plastiki katika maziwa na bahari ukilinganisha na Samaki ifikapo mwaka 2050.

Bahati Mayoma ni Mhadhiri Msaidizi wa Shule kuu ya Sayansi Akua na Teknolojia za uvuvi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam, anasema taka ngumu kama plastiki sio Rafiki wa mazingira hususani kwa viumbe hai waishio chini ya maji.

“Ongezeko la taka za plastiki katika maeneo ya Bahari na Ziwa yanaleta athari nyingi za moja kwa moja na zile ambazo siyo za moja kwa moja, kwasababu hizi taka ambazo zinatupwa kwenye vyanzo vya maji zinapelekea uhusiano hasi kati ya Samaki na hizi taka”.

“Baadhi ya viumbe hasa Samaki wanameza hivi vipande vya plastiki na wanapovimbeza kumbuka haviwezi kumeng’enywa kwasababu vimeundwa kwa kemikali ambazo haziwezi kumeng’enywa,kwa hiyo zinaziba mifumo ya chakula ya Samaki”.

“kwahiyo hawa Samaki badala ya kuhisi wana njaa, wanahisi wameshiba na kuwafanya wadhoofike na wengine wanakufa, kwa hiyo plastiki wanaathiri Samaki kwa namna hiyo”, alisema Mayoma.

Bahari ni makazi ya kiwango kikubwa cha bayonuai. Pichani ni mwanamke huyu mkazi wa Entebbe, Uganda, akiwa ziwa Victoria, ziwa ambalo linatumiwa kwa pamoja na nchi za Uganda, Tanzania na Uganda.
Arne Hoel/World Bank
Bahari ni makazi ya kiwango kikubwa cha bayonuai. Pichani ni mwanamke huyu mkazi wa Entebbe, Uganda, akiwa ziwa Victoria, ziwa ambalo linatumiwa kwa pamoja na nchi za Uganda, Tanzania na Uganda.

Serikali imeonya nini kuzuia taka za plastiki zisiingie ndani ya vyanzo vya maji?

Umoja wa Mataifa ulitenga siku maalumu ya kuondoa taka ikilenga kuzuia matumizi endelevu na mifumo ya uzalishaji, kuunga mkono mabadiliko ya jamii na kuongeza ufahamu kuhusu jinsi mipango ya kutoondoa taka inavyochangia katika kuendeleza ajenda ya maendeleo endelevu ya umoja wa mataifa ifikapo mwaka 2030.

Hata hivyo serikali ya Tanzania imekuwa ikitoa elimu ya utunzaji wa mazingira ikiwemo maeneo ya fukwe huku ikihasisha wananchi kuzigeuza taka kuwa bidhaa ili kujipatia kipato.

Afisa Usafirishaji na Mazingira kutoka Manispaa ya Ilemela Jijini Mwanza nchini Tanzania Nyabugumba Jonathan anawaasa wavuvi na watumiaji wa fukwe kutunza maeneo.

“Bado tunahitaji kuhamasishana, tunaona kuna takataka za plastiki, chupa, mali chakavu zipo katika fukwe, nichukue fursa hii kuwaomba tuendelee kuyatunza mazingira haya”.

“Lakini leo mmepata elimu ya namna gani mnaweza kubadilisha taka kama hizi za plastiki na kuwa bidhaa, jaribuni kutumia elimu hii ili muweze kujipatia kipato kitakacho wawezesha kuendesha familia zenu lakini na serikali pia itapata kodi”, alisema Jonathan.

Umoja wa Mataifa katika kukabiliana na Tatizo hilo duniani, ilianzisha siku ya kutozalisha na kutupa taka, huku ikiwataka wadau wote ikiwa ni pamoja na serikali, mashirika ya kiraia, wafanyabiashara, wanazuoni, wanawake, na vijana kushiriki katika shughuli zinazoongeza ufahamu wa mipango ya kuondoa Taka.

 

Makala hii imeandikwa na Evarist Mapesa wa radio washirika SAUT FM iliyoko mkoani Mwanza nchini Tanzania.