Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Miaka 20 ya kuchunguza maiti ili kuleta nuru kwa familia

UNHCR/S.Baltagiannis
Wahamiaji wanaosaka maisha bora wengine wakinusurika kifo kama mtoto mkimbizi huyu akiwa amepumzika katika kisiwa cha Lesvos huko Ugiriki wakisubiri kufahamu hatma yao ya kuhamishiwa. (Picha: © UNHCR/S.Baltagiannis)

Miaka 20 ya kuchunguza maiti ili kuleta nuru kwa familia

Wahamiaji na Wakimbizi

Profesa mmoja nchini Ugiriki ameamua kutumia ubobezi wake wa utambuzi wa maiti ili kuweza kuwaunganisha na ndugu zao baada ya ndoto zao za kusaka maisha bora Ulaya kuishia kwenye mto mmoja unaotenganisha Ugiriki na Uturuki.

Pavlidis Pavlos wa Chuo Kikuu cha Democritus, nchini Ugiriki hufanya kazi hiyo kwa kutumia maiti walioopolewa kutoka mto Evros upande wa Ugiriki.

Akizungumza na maafisa wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR waliotembelea ofisi yake, Profesa Pavlos amesema wanatumia vitu kadhaa kupima na kubaini utambulisho wa maiti ikiwemo mabaki ya nguo, pete, simu hata nywele.

“Napenda kazi yangu na nafurahi sana pindi ninapoweza kufuta angalau machozi ya familia kwa kuwaletea mwili wa ndugu yao ambaye walikuwa hawajui alipo,” amesema Profesa huyo ambaye tangu mwaka 2000 hadi mwaka jana amechunguza maiti 359 kutoka mto Evros.

Amesema mwaka huu pekee ameshachunguza maiti 12 ambapo kila mwili hukaa kwenye jokofu kwa kati ya miezi mitatu hadi saba.

Kwa mujibu wa Profesa Pavlos tangu wakati huo ameweza kutambua miili 103 ambapo familia wameweza kuchukua maiti wao kwa maziko.

Ametaja sababu kuu ya vifo kuwa ni kuzama kwenye maji na wengine wanafariki dunia kwa sababu ya baridi kali huku wengine wakiwa wamepata ajali.

Kuhusu changamoto, Profesa huyo amesema “ si kazi rahisi kwa kuwa mwili huharibika haraka kwenye maji baridi kuliko kwenye maji ya chumvi, kwa hiyo nyaraka za utambulisho zinaharibika, simu za kiganjani halikadhalika na miili kwa hiyo inakuwa vigumu sana kutambua.”