Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashine kutoka ITC yawezesha wanawake Buhigwe kukamua mawese kwa saa 1 badala ya saa 8

Wanawake wa kata ya Janda, wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma nchini Tanzania wakitazama jinsi wafanyakazi kutoka SIDO na kituo cha biashara cha kimataifa, ITC wakiendesha mtambo wa kisasa wa kukamua mafuta ya mawese, ambao wanawake hawa watatumia badala ya
ITC VIDEO
Wanawake wa kata ya Janda, wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma nchini Tanzania wakitazama jinsi wafanyakazi kutoka SIDO na kituo cha biashara cha kimataifa, ITC wakiendesha mtambo wa kisasa wa kukamua mafuta ya mawese, ambao wanawake hawa watatumia badala ya kutumia mashine ya kukamua kwa mikono.

Mashine kutoka ITC yawezesha wanawake Buhigwe kukamua mawese kwa saa 1 badala ya saa 8

Ukuaji wa Kiuchumi

Mradi wa pamoja wa Kigoma, KJP nchini Tanzania unaoendeshwa na mashirika ya Umoja wa Mataifa umeendelea kuwa baraka kwa wakazi wa mkoa huo ambapo wanufaika wa hivi karibuni zaidi ni kikundi cha wanawake kata ya Janda wilaya ya Buhigwe, kilichopatiwa kiwanda kidogo cha kuchakata mafuta ya mawese, na hivyo kuondokana na njia ya kienyeji.  

Wanawake hao wamekabidhiwa mashine hiyo iliyotengenezwa na shirika la viwanda vidogo SIDO mkoani Kigoma kwa ufadhili wa kituo cha biashara cha kimataifa, ITC, kupitia mradi wa uwezeshaji vijana na wanawake, YWEE wa KJP.

Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe Kanali Michael Ngayalina alishuhudia jinsi wanawake hao walikamua mafuta kwa saa moja badala ya saa 8 ambazo huhitajika wakati wa kukamua kwa kutumia mashine ya kienyeji.

Teddy Mayaya ambaye ni Afisa Kilimo kata ya Janda amesema kuwa, kwa kweli kabla ya kupatiwa hii mashine kulikuwa na hali ya ngumu kwa sababu mashine zilizokuwa zinatumika ni hizi za kienyeji ambazo zinatumia muda mrefu na muda mwingi na mafuta hayakuwa bora kama kuchakata mafuta kwenye kiwanda hiki walichopatiwa sasa hivi.Kukamua mafuta kwa mashine hizi za kienyeji inachukua muda kwa sababu inabidi  uzivundike kama muda wa siku mbili au tatu, baadaye uzikatekate na baadaye uweke kwenye pipa upike ndio uje upate Mafuta. Kwa hiyo inachukua muda kama siku tatu au nne ”

Mfanyakazi kutoka SIDO akiendesha mtambo huo wa kukamua mafuta ya mawese, mtambo ambao umetengenezwa na SIDO kwa ufadhili wa ITC
ITC VIDEO
Mfanyakazi kutoka SIDO akiendesha mtambo huo wa kukamua mafuta ya mawese, mtambo ambao umetengenezwa na SIDO kwa ufadhili wa ITC

Lakini kwa wanakikundi ni tofauti gani wanaona, Neema Milembe ni mmoja wao na anaangazia ubora wa mafuta akisema kuwa, “kwanza kuna ongezeko, mafuta ambayo yamekamuliwa hapa kwa mashine yanakuwa na zidio kidogo kuliko yale ya kukamua kwa kutumia mikono, na pia ubora uko zaidi sana kuliko yale ya kukamua kwa mikono.”

Dorice Musa ni mwanakikundi ambaye pamoja na shukrani anasema “lakini wangetusaidia umeme, usumbufu ungekuwa mdogo, pia tunaomba watuletee mashine ya kusaga mafua ya mise, tupanue wigo ili tutengeneze sabuni.”..

Kwa Agnes Buharisha, ujumbe kwa ITC ni kwamba, “hiki walichokifanya waendelee kufanya ili changamoto zipungue kwa kila mmoja atakayekwenda kutumia mashine hii, changamoto za maji, maji yapo lakini ni ya mgao, hayatoshi kijijini. Kwa hiyo inaonekana tutakuwa tunafuatilia maji kama zamani, na hii italeta usumbufu, na hii itasaidia wale wateja wanaokuja kusagisha na wanawake walioanzisha vikundi.”

Kufuatia makabidhiano hayo kiwanda hicho, wanakikndi watapatiwa mafunzo ya namna ya kukiendesha na kibiashara kwa kuongeza mnyororo wa thamani katika kutengeneza sabuni na kupata mashudu ya wanyama kwa kukamua mafuta ya mise.