Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mafunzo ya kilimo cha kutumia wanyamakazi yaleta nuru kwa vijana Kigoma

Vijana katika mkoa wa  Kigoma ulioko Kaskazini-magharibi mwa Tanzania wakiwa kwenye mafunzo ya kulima kwa kutumia wanyamakazi ikiwa ni mradi wa kufanikisha kilimo bora na kujipatia kipato.
FAO Tanzania
Vijana katika mkoa wa Kigoma ulioko Kaskazini-magharibi mwa Tanzania wakiwa kwenye mafunzo ya kulima kwa kutumia wanyamakazi ikiwa ni mradi wa kufanikisha kilimo bora na kujipatia kipato.

Mafunzo ya kilimo cha kutumia wanyamakazi yaleta nuru kwa vijana Kigoma

Ukuaji wa Kiuchumi

Mafunzo yaliyoendeshwa na shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo duniani, FAO  nchini Tanzania kwa vijana wakulima wilayani Kakonko mkoani Kigoma yameleta nuru ya kujiajiri na kujipatia kipato wakati huu ambapo Umoja wa Mataifa unataka vijana wasiachwe nyuma katika kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs.  

Wakulima vijana wamefundishwa kuhusu Kilimo cha kutumia jembe linalokokotwa na wanyama kazi ambayo ni mbinu ngeni kwa wakazi wengi wa Mkoa wa Kigoma hususani wenyeji asilia.   
 
MAfunzo yalitolewa kwa ushirikiano kati ya FAO na asasi isiyo ya kiserikali ijulikanayo kama Nyakitoto Youth For Development In Tanzania (NYDT) pamoja na Halmashauri ya Wilaya za Kakonko, Kasulu na Kibondo vijana wakulima kutoka kaya zenye Ngo’mbe waliainishwa na kupatiwa mafunzo kwa vitendo kuwaongoza ng’ombe kukokota jembe la kulimia. 

Juma Salehe mmoja wa vijana wanufaika anasema, “nina furaha kwani nimeona mwanga mbele wa kujiajiri na kujipatia kipato”.  

Juma mkazi wa Kakonko Mkoani kigoma nchini Tanzania amesema mafunzo ya kuwaongoza wanyamakazi katika kuandaa shamba kabla ya Kupanda yamekuwa ufunguo wa maisha yake akishuruku FAO kwa kugharimia mafunzo kupitia mradi wa Pamoja wa Kigoma, KJP unaofadhiliwa na serikali ya Norway. 
 
Juma anasema,“nitawafundisha na kuwahamasisha vijana wenzangu kulima kwa kutumia jembe linalokokotwa na ngo’mbe.”   
 
Mkulima mwezeshaji Masanja Manyama kutoka Shinyanga amekiri kuwa vijana hao kutoka kata ya Nyabibuye wilayani Kakonko wamefuzu. 
 
Akifurahia Mafunzo hayo Gabriel Bahati alikiri kwamba uzoefu alioupata utamsaidia kutoa huduma kwa jamii na wakati huo huo kujipatia kipato akiongeza kuwa“ kwa sasa ekari moja kwa kutumia jembe la mkono hulimwa kwa gharama ya kati ya Shilingi elfu arobaini hadi sitini na huhusisha watu wengi na huchukua takriban siku 4 hadi 6 kumaliza. Kwa kutumia jembe linalokokotwa na ngómbe ekari moja humalizika kwa masaa machache ndani ya siku moja na kuhitaji watu wawili tu.Nitaweza kulima kwa shilingi 30,000 kwa eka moja ambayo nitaimaliza kwa muda mfupi na kujipatia kipato”  
 
Naye Afisa ugani wa Kata ya Nyabibuye Philbert Kassano alionesha kufurahishwa na kuletwa kwa mbinu hii na amesema “huduma hii italeta tija katika wanakijiji na naomba Halmashauri ipanue wigo wa huduma hii na mafunzo haya katika Kata na vijiji vingine ili vijana wajipatie ajira lakini pia kuhudumia eneo la uzalishaji wa mazao kwa muda mfupi.”