Skip to main content

Kama tunamuenzi Mandela, basi tuzingatie usawa- Guterres

Katibu Mkuu wa UN António Guterres akihutubia mhadhara wa kila mwaka wa Nelson Mandela
UN/Eskinder Debebe
Katibu Mkuu wa UN António Guterres akihutubia mhadhara wa kila mwaka wa Nelson Mandela

Kama tunamuenzi Mandela, basi tuzingatie usawa- Guterres

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Ukosefu wa usawa, suala ambalo linaainisha zama zetu za sasa, linahatarisha kusambaratisha chumi za dunia na jamii hivi sasa, amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres katika hotuba yake aliyoitoa jijini New York, Marekani hii leo katika kuadhimisha Mhadhara wa Nelson Mandela kwa mwaka 2020.

Mhadhara huo umefanyika hii leo ikiwa ni siku aliyozaliwa hayati Nelson Mandela, rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini, na ni kwa mara ya kwanza umefanyika kwa njia ya mtandao kutokana na janga la ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19.

Lengo la tukio hilo linalosimamiwa na taasisi ya Nelson Mandela ni kuchagiza mashauriano kwa kualia watu mashuhuri kujadili changamoto za kimataifa.

COVID-19 imetuanika

Mama akiwafundisha wanae katika wilaya ya Shamva nchini Zimbabwe wakati wa mlipuko wa COVID-19.
WFP/Tatenda Macheka
Mama akiwafundisha wanae katika wilaya ya Shamva nchini Zimbabwe wakati wa mlipuko wa COVID-19.

 

Katibu Mkuu alianza hotuba yake kwa kutambua jinsi janga la COVID-19 limekuwa na dhima kubwa katika kuangazia ukosefu wa usawa duniani na kutengua usemi ya kwamba kila mtu yuko kwenye mashua moja kwa sababu “sote tunaogelea kwenye bahari moja” ambapo amesema ni dhahiri kuwa baadhi ya watu wako kwenye mashua za kisasa, ilhali wengine wanaelea kwenye taka.

Wakati sote tunaogelea kwenye bahari moja, ni dhahiri kuwa wengine wamo ndani ya mashua za kisasa huku wengine wakielea juu ya taka   -    António Guterres, Katibu Mkuu, Umoja wa Mataifa.

Hatari za dunia zilizopuuzwa kwa miongo kadhaa, mathalani mifumo ya afya iliyo dhaifu, pengo katika hifadhi ya jamii, mifumo ya ukosefu wa usawa, uharibifu wa mazingira na janga la tabianchi yako bayana, amesema Katibu Mkuu akiongeza kuwa, “wale walio hatarini ndio wanataabika zaidi: wanaoishi kwenye umaskini, wazee, watu wenye ulemavu na wenye magonjwa.”

Bwana Guterres amesema kuwa ukosefu wa usawa uko katika aina nyingi. Wakati tofauti za kipato ni bayana, ambapo asilimia 26 ya matajiri duniani wanashikilia utajiri wa nusu ya idadi ya watu wote duniani, fursa za maisha pia zinategemea vigezo kama vile, jinsia, familia, kabila, rangi na iwapo mtu ana ulemavu au la.

Hata hivyo amesema kuwa, kila mtu anapata madhara ya hali hiyo, kwa sababu viwnago vya juu vya ukosefu wa usawa vina uhusiano na ukosefu wa utulivu kwenye uchumi, majanga ya kifedha, ongezeko la uhalifu na afya dhoofu ya mwili na akili.

Athari za ukoloni bado zipo

Maandamano yamekuwa yakifanyika katika miji kote Marekani ikiwa ni pamoja na jiji la New York kudai kuzingatiwa kwa haki za wamarekani weusi.
UN /Shirin Yaseen
Maandamano yamekuwa yakifanyika katika miji kote Marekani ikiwa ni pamoja na jiji la New York kudai kuzingatiwa kwa haki za wamarekani weusi.

 

Katibu Mkuu ameibua pia suala la ukoloni, akisema ni jambo la kihistoria ambalo limechochea ukosefu wa usawa.

Bwana Guterres amesema, “harakati dhidi ya ubaguzi wa rangi tunazoshuhudia sasa, zinaainisha chanzo cha kihistoria cha ukosefu wa usawa. Mataifa ya kaskazini, hususan bara langu mwenyewe la Ulaya, lilitawala nchi nyingi za kusini  kwa miongo kadhaa, kwa mabavu na vita. Hii ilisababisha ukosefu wa usawa ndani ya nchi, baina ya nchi ikiwemo biashara ya utumwa kupitia bahari ya Atlantiki na utawala wa kibaguzi huko Afrika Kusini.”

Amesema vitendo hivyo vimeacha alama ya ukosefu wa haki za kijamii na kiuchumi, uhalifu utokanao na chuki, chuki dhidi ya wageni, mfumo wa ubaguzi wa rangi na ubora wa watu weupe.

Mfumo dume

Bwana Guterres pia amegusia mfumo dume, msingi mwingine wa kihistoria kwenye ukosefu wa usawa, akisema bado upo kwa kuwa kila mahali, wanawake wako katika hali mbaya kuliko wanaume na ukatili dhidi ya wanawake umefikia kiwango cha janga.

Akijitambulisha mwenyewe kama mtetezi wa wanawake anayejivunia, Katibu Mkuu amesema ameazimia kusimamia usawa wa kijinsia na suala la usawa wa jinsia amelizingatia katika uteuzi wake wa nafasi andamizi ndani ya Umoja wa Mataifa.

Halikadhalika ametumia hotuba yake kutangaza kuteuliwa kwa mcheza raga wa Afrika Kusini, Siya Kolisi, kuwa bingwa wa dunia wa mpango wa Spotlight, ambao unalenga kujumuisha wanaume katika vita dhidi ya ukatili wanaofanyiwa wanawake na wasichana.

Kila mtu lazima alipe kodi stahili

 

Moshi wa magari, jenereta za dizeli na kuchoma taka na samadi vimesababisha uchafuzi wa hewa kwenye mij wa Lagos nchini Nigeria kama inavyoonekana kwenye picha hii ya mwaka 2016
© UNICEF/Bindra
Moshi wa magari, jenereta za dizeli na kuchoma taka na samadi vimesababisha uchafuzi wa hewa kwenye mij wa Lagos nchini Nigeria kama inavyoonekana kwenye picha hii ya mwaka 2016

 

Akigeukia ukosefu wa usawa wa zama za sasa, Bwana Guterres amesema kupanuka kwa biashara, maendeleo ya teknolojia vimechangia katika mabadiliko yasiyotarajiwa ya mgao wa vipato. “Watu wenye stadi za chini wanabeba mzigo, na wanakabiliwa na shambulizi kutoka teknolojia mpya, ajira zisizohitaji binadamu, uzalishaji wa mbali na kutoweka kwa vyama vya wafanyakazi.”

Wakati hayo yakiendelea, amesema, “misamaha ya kupindukia ya kodi, viwango vya chini vya kodi kwa kampuni, ni kumaanisha kuwa ni punguzo la wigo wa rasilimali zinazotakiwa kwa ajili ya hifadhi ya jamii, elimu, huduma za afya, mambo ambayo ni muhimu katika kupunguza ukosefu wa usawa.”

Amesema kuwa baadhi ya nchi zimeruhusu matajiri na wale wanaofahamiana na watu wakubwa kunufaika na mifumo ya kodi, lakini, “kila mtu lazima alipe kodi anayostahili,” amesema Katibu Mkuu na kwamba serikali lazima zishughulikia janga lililoota mizizi la ufisadi, ambalo linadhoofisha maadili ya kijamii na utawala wa sheria na wakati huo huo , serikali hizo ziondoe mzigo wa kodi kwenye mishahara na zipeleke kwenye hewa ya ukaa.

“Kwa kufanya hivyo itasaidia kushughulikia janga la tabianchi,”  amefafanua Bwana Guterres.

Makubaliano mapya ya dunia

Mafuriko makubwa katika eneo la pembe ya Afrika na Kenya yamesababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu ikiwemo barabara.
UN Photos
Mafuriko makubwa katika eneo la pembe ya Afrika na Kenya yamesababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu ikiwemo barabara.

Ijapokuwa mabadiliko ya tabianchi ni tatizo la dunia, madhara yake yanagusa nchi zile ambazo mchango wake ni mdogo sana kwenye hali ya sasa na kwamba hali itakuwa mbaya zaidi siku za usoni pindi mamilioni ya watu watakapokabiliwa na utapiamlo, malaria na magonjwa mengine, uhamaji wa lazima na hali mbaya ya hewa ya kupitiliza.

Katibu Mkuu amesema njia pekee kuelekea mustakabali wenye usawa na endelevu ni kuwa na mkataba mpya wa kijamii ambao unaruhusu vijana kuishi maisha ya utu, wanawake kuwa na fursa sawa na matumaini kama wanaume na kuwalinda wale walio hatarini zaidi. “Mkataba mpya wa dunia ambao unahakiksha kuwa mamlaka, utajiri na fursa zinatumiwa katika wigo mpana zaidi na kwa usawa katika ngazi za kimataifa,”  amesema Katibu Mkuu.

Hata hivyo amesema, katika mkataba huo, sera a ajira zitazingatia mashauriano ya kina na yenye maana kati ya mwajiri na mwajiriwa, na kuhakikisha haki za binadamu na aina zote za uhuru vinazingatiwa.

“Natoa wito wa kuwepo kwa mifumo mpya ya hifadhi ya jamii, ikiwemo huduma ya afya kwa wote, UHC, uwekezaji zaidi katika huduma za umma na kubadili ukosefu wa usawa, na kuweka hatua za upendeleo na sera nyingine za kushughulikia ukosefu wa usawa kwa misingi ya jinsia na kabila,”  amesema Bwana Guterres.

 

Wanafunzi wa wakiwa darasani katika shule ya msingi ya Zanaki jijini Dar es Salaam nchini Tanzania
World Bank / Sarah Farhat
Wanafunzi wa wakiwa darasani katika shule ya msingi ya Zanaki jijini Dar es Salaam nchini Tanzania

Katibu Mkuu ameeleza kuwa elimu bora kwa wote, matumizi mapana ya teknolojia ,vitakuwa muhimu katika kufanikisha malengo hayo.

“Hii inamaanisha kuongeza maradufu bajeti ya elimu katika nchi za vipato vya chini na vya kati ili ifikie dola trilioni 3 kwa mwaka hadi ifikapo mwaka 2030: ndani ya kizazi, watoto wote katika nchi za vipato vya chini na kati wataweza kuwa na elimu bora katika ngazi zote,”  amefafanua Katibu Mkuu.

Hata hivyo ameseam ni muhimu serikali zibadili mbinu za kufundisha watoto akisema kuwa, kuwekeza kwenye elimu ya dijitali na miundombinu yake na kuwasaidia kujiandaa kwa mabadiliko ya hali ya juu ya ufanyaji kazi ambao unabadilishwa na teknolojia.”

‘Tusimame pamoja, au tusambaratike’

 

Hafla ya kufunga mjadala wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na rais wa Baraza Kuu Tijjani Muhammad-Bande. Septemba 30, 2019
UN Photo/Cia Pak
Hafla ya kufunga mjadala wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na rais wa Baraza Kuu Tijjani Muhammad-Bande. Septemba 30, 2019

Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa ametamatisha hotuba yake ya kimkakati na maono kwa kuibua umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa na mshikamano.
“Sisi ni wamoja, tusimame pamoja au tusambaratike,” amesema Katibu Mkuu akiongeaza kuwa dunia ipo katika njia panda, ni wakati wa viongozi kuamua njia ya kufuata. 

Chaguo la Bwana Guterres ni kati ya “vurugu, mgawanyiko na ukosefu wa usawa” au kushughulikia makosa yaliyopita na kusonga mbele pamoja na kwa maslahi ya wote.