Tukimuenzi Mandela tusimamie maadili yake na kuziba pengo la usawa:UN

16 Julai 2020

Katika kuelekea siku ya kimataifa ya Nelson Mandela hapo Jumamosi Julai 18, siku ya kuzaliwa kwa mwanaharakati huyo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema ni muhimu kumuenzi kwa kupigania maadili yake kama kuziba pengo la usawa.

Kupitia ujumbe wake wa siku hiyo ya Mandela , Guterres amesema ni ya kutoa heshima kwake kama mtetezi wa ulimwengu wenye usawa, utu na mshikamano.

Na kuongeza kuwa Madiba alikua kielelezo cha maadili kwa karne ya 20, ambaye urithi wake usiokoma unaendelea kuiongoza dunia hata leo.Kauli mbiu ya Siku ya Kimataifa ya Nelson Mandela ni “Chukua hatua, hamasisha mabadiliko” ikiaangazia umuhimu wa kufanya kazi kwa pamoja, kuanzia kwa serikali hadi raia, na kujenga dunia yenye amani, endelevu na yenye usawa. Kwa mantiki hiyo Katibu Mkuu amesemaTunaadhimisha siku hii wakati ambapo tishio la janga la COVID-19 linahatarisha kila mtu, kila mahali, na hususani walio hatarini zaidi. Kwa kukabiliwa na changamoto hizi, viongozi ulimwenguni wanahitaji kutambua umuhimu wa umoja na mshikamano. COVID-19 imeibua ukosefu wa usawa wa kupindukia.

Amesisitiza kuwa ni lazima kupigana na janga hili la ukosefu wa usawa kupitia mkataba mpya wa kijamii kwa ajili ya enzi mpya akiamini kwamba kwa pamoja tunaweza kulishinda tishio tulilonalo la COVID-19. Bwana  Guterres amekumbusha kwamba wakati Umoja wa Mataifa unaadhimisha kumbukumbu ya miaka 75 wakati huu dhaifu, ni muhimu kutafakari juu ya maisha na kazi ya Nelson Mandela, ambaye aliheshimu maadili ya Umoja wa Mataifa na ambaye alichukua hatua na kuchagiza mabadiliko.

Na kwamba licha ya kuwa mfungwa wa dhamira kwa miaka mingi, Madiba aliboresha utu wake na kujitolea kwa maoni yake. Ametaka mfano wake uzingatiwe na serikali yeyote ile inayoweka wafungwa wa aina hiyo na iwaachie kwani hatupaswi kuwa na wafungwa wa dhamira katika karne ya 21.“Nelson Mandela alitukumbusha kwamba: “Kadiri umaskini, ukosefu wa haki na wa usawa ukiendelea ulimwenguni, hakuna yeyote anayeweza kuwa na mapumziko ya kweli. Katika Siku hii ya Mandela, tukumbuke kuwa tunaweza, na lazima kuwa sehemu ya mustakabali bora, fursa na ustawi kwa watu wote kwenye sayari yetu imara.”

Marianna V. Vardinoyannis, Mshindi wakike aliyeshinda tuzo la Umoja wa Mataifa la 2020 Nelson Rolihlahla Prize.
United Nations

Kila baada ya miaka mitano katika maadhimisho ya siku ya Mandela hutolewa tuzo ijulikanayo kama Mandela Priza kwa heshma ya kumuenzi mtetezi huyo wa haki duniani kwa watu ambao wamefuata nyayo zake kwa vitendo na mwaka huu waliobahatika kuitwaa tuzo hiyo ni Marianna Vardinoyannis  kutoka Ugiriki  Rais wa wakfu wa Marianna Vardinoyannis unaosaidia watoto wenye saratani na zaidi na Dkt. Morissanda Kouyate kutoka Guinea ambaye ni mkurugenzi mtendaji wa kamati ya Afrika inayohusika na mila na tamaduni zinazoathiri afya ya wanawake na watoto.

Morissanda Kouyate, mwanaume mshindi wa tuzo la 2020 la Umoja wa Mataifa la Nelson Rolihlahla Mandela Prize.
United Nations

 

Washindi hawa wote wawili ni watetezi wa masuala ya kibinadamu. Akiwapongeza hii leo katika tukio maalum la kumuenzi Mandela kwenye Umoja wa Mataifa wakati huu wa janga la COVID-19 Rais wa Baraza Kuu Tijjan Muhammad-Bande amesema“Leo hii tukipambana na janga la COVID-19, tukipambana na pengo la usawa ambalo pia limeongeza zahma kwa janga hili, pia tunazungumzia vuguvugu la kijamii kote duniani na usawa duniani kote. Nafikiri kwa mara nyingine hii inatoa picha iliyo wazi kwa misingi ya maisha na kazi ya Mandela ambayo naweza kusema nyie wote wawili mnaiendeleza kazi hiyo.”

 

 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter