Huduma za posta zaenda sambamba na kasi ya ukuaji wa teknolojia- UPU
Huduma za posta zaenda sambamba na kasi ya ukuaji wa teknolojia- UPU
Shirika la posta duniani, UPU, limetaka maadhimisho ya siku ya posta duniani hii leo yatumike kutathmini jinsi ambavoy shirika hilo lililoanzishwa miaka 145 iliyopita limechangia katika kusongesha utu na maendeleo.
Katika ujumbe wake wa siku hii leo, Mkurugenzi Mkuu wa UPU Bishar Hussein amesema hiyo ndio njia pekee ya kusherekea yaliyopita kwa kuangazia ni jinsi gani shirika hilo litakuwa bora zaidi siku za usoni katika kutoa huduma zake.
“Tumekuwa tukiongozwa kwenye kazi hii kwa kuzingatia mahitaji ya binadamu katika kukabiliana na changamoto zao ili tuweze k uhakikisha kuwa tuna mustakabali tuutakao katika sayari yetu,” amesema Bwana Hussein.
Amesema mwelekeo huo ndio njia bora zaidi ya kutoa huduma za maendeleo kwa dunia ya sasa.
Mathalani amesema kutokana na kasi ya maendeleo, huduma za posta nazo zimeendelea kuwa bunifu kuanzia kupokea barua kutoka kwa mtumaji, kuzichambua, kuzituma na kuziwasilisha kwa mhusika.
“Kwa kukumbatia teknolojia za kisasa kama vile maroboti na mitando ya intaneti, posta hii leo imeweza kwenda na wakati katika utoaji wa huduma zake kwa wateja. Hivi sasa tuko karibu zaidi na wateja kuliko nyakati za awali,” amesema Mkurugenzi Mkuu wa UPU.
Ubunifu wowote unaendelea kuzingatia msingi wa uwepo wetu
Hata hivyo amesema, falsafa ya awali kabisa ya UPU ya kuhudumia binadamu na kufanikisha mawasiliano, inasalia kuwa kichocheo kikubwa katika mtandao wa posta duniani.
“Ubunifu wowote ule kwenye huduma za posta unalenga kufanikisha sababu yetu ya awali ya uwepo wetu; kufanya maisha ya watu yawe bora zaidi,” amesema Bwana Hussein.
Amesema mitandao ya posta iwe ile iliyoendelea, inayoendelea na iliyoko mbali zaidi kiteknolojia, inaendelea kushirikiana na kuwa na uwezo wa kufikisha huduma bora zaidi na kwa bei nafuu kwa wakazi wa dunia.