Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu 11 wakiwemo wanawake na watoto wameuawa katika shambulio la anga Yemen:OCHA

Mazingira ya Cratar huko Aden, Yemen. (18 Novemba 2018)
OCHA/Giles Clark
Mazingira ya Cratar huko Aden, Yemen. (18 Novemba 2018)

Watu 11 wakiwemo wanawake na watoto wameuawa katika shambulio la anga Yemen:OCHA

Amani na Usalama

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu misaada ya kibinadamu na masuala ya dharura OCHA limesema taarifa kutoka Yemen zinasema kwamba shambulio la anga lililofanyika jana Jumatano Julai 15 limekatili maisha ya watu 11 wakiwemo wanawake na watoto na kujeruhi raia wengine 6.

Shambulio hilo lililofanyika katika eneo la Al Musaafah Al Maraziq Mashariki kwenye jimbo la Al Jawf, Kaskazini mwa Yemen ni la pili ndani ya siku tatu  na majeruhi ni watoto watano na mwanamke mmoja.Kwa mujibu wa mratibu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa Yemen Lise Grande idadi kamili ya vifo na majeruhi inaweza kuwa kubwa zaidi. Majeruhi wameumia vibaya sana na imebidi kukimbizwa hospitali mjini Sana’a kwa matibabu. “Kwa mara ya pili wiki hii wanawake na watoto wameuawa kikatili na kujeruhiwa katika shambulio. Tunatuma salamu zetu za rambirambi kwa wanaoomboleza msiba huo na kuwaombea nafuu ya haraka majeruhi. Hili ni shambulio la pili ndani ya siku tatu linalosababisha maafa makubwa kwa raia.” 

Amesema Bi. Grande na kuongeza kwamba mnamo Julai 12 shambulio la anga liliua raia tisa na kujeruhi wengine 4 katika jimbo la Hajjah Kaskazini Maharibi mwa Yemen.Amekumbusha kwamba katika kipindi cha miezi 6 ya mwanzo ya mwaka 2020 kumekuwa na vifo na majeruhi zaidi ya 1,000 kutokana na mgogoro unaoendelea Yemen.“Tunachokishuhudia ni ukatili wa kupindukia, njia pekee ambayo itawafanya raia wa Yemen kuwa salama ni pale ambapo pande kinzani zitakapoamua kukomesha uhasama. Wahudumu wa kibinadamu kwa muda mrefu wamekuwa wakitoa wito wa kusitisha mapigano, hivyo fursa pekee kwa watu wa Yemen ni kwa pande hizo kinzani kuchukua hatua sasa.”

Kwa mujibu wa OCHA Yemen inasalia kuwa ndio mgogoro mbaya zaidi wa kibinadamu duniani ambapo karibu asilimia 80 ya watu wote nchini humo ambao ni zaidi ya milioni 24 wanahitaji aina moja au nyingine ya msaada wa kibinadamu na ulinzi.Na kati ya dola bilioni 2.41 zinazohitajika kukidhi mahitaji ya kibinadamu nchini humo hadi mwisho wa mwaka huu ni dola bilioni 1.35 pekee ndizo zilizopatikana na hivyo kuacha pengo kubwa la dola zaidi ya bilioni moja.Sababu ya ukata mashirika mbalimbali ya Umoja wa Mataifa  Yemen yamelazimika kufunga programu 31 kati ya 41 za misaada ya kibinadamu tangu mwezi Aprili.