Watoto 7 na wanawake 2 wauawa katika shambulio jimboni Hajjah Yemen:OCHA

13 Julai 2020

Taarifa za awali kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu misaada ya kibinadamu na masuala ya dharura OCHA inasema shambulio la anga lililofanyika jana tarehe 12 Julai katika wilaya ya Washhah jimbo la Hajjah Kaskazini Magharibi mwa Yemen limekatili maisha ya watoto saba, wanawake wawili na kujeruhi raia wengine wanne.

Katika taarifa ya shirika hilo iliyotolewa leo majeruhi ni atoto wawili na wanawake wawili ambao wote sasa wanapatiwa matibabu katika hospitali ya Abs.

Akilaani vikali shambulio hilo mratibu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya kibinadamu Yemen Lise Grande amesema “Inasikitisha na kughadhibisha kwamba katikati ya janga la corona au COVID-19 wakati mjadala wa usitishwaji uhasama uko mezani raia wanaendelea kuuawa Yemen. Tunatuma rambirambi zetu kwa familia na jamaa wa watoto na wanawake ambao waliuawa katika shambulio hilo na kuwatakia ahuweni ya haraka majeruhi.”

UN Photo/Isaac Billy
Mratibu wa Huduma za Kibinadamu wa UN nchini Yemen, Lise Grande kwenye mkutano na waandishi wa habari.

Bi. Grande ameongeza kuwa kumekuwa na vifo na majeruhi karibu 1,000 nchini Yemen katika miezi sita ya mwanzo wa mwaka 2020 hivyo amesisitiza “Yemen haiwezi kumudu vifo zaidi. Hakuna ufadhili wa kutosha , program za huduma za afya na maji zinafungwa, baa la njaa linainyemelea Yemen tena na watu kote nchini wameathirika vibaya na COVID-19. “

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa Yemen inasalia kubwa mgogoro mbaya zaidi wa kibinadamu duniani ambapo karibu asilimia 80 ya watu wote milioni 24 wa nchi hiyo wanahitaji aina fulani ya msaada wa kibinadamu na ulinzi.

Katika mkutano wa kimataifa wa uchangishaji fedha kwa ajili ya Yemen uliofanyika Riadhi Juni pili mwaka huu wahisani waliahidi dola bilioni 1.35 kati ya dola bilioni 2.41 zinazohitajika kukidhi mahitaji ya kibinadamu kwa taifa hilo hadi mwisho wa mwaka huu na hivyo kuacha pengo la zaidi ya dola bilioni 1.

Tangu katikati ya mwezi Aprili mwaka huu program 31 za Umoja wa Mataifa za misaada kati ya program 41 zimepunguza kazi au kufungwa kabisa kutokana na ukata.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter