Michoro ya mitaani yatumika kuelimisha umma kuhusu COVID-19 Niger

14 Julai 2020

Nchini Niger, shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji, IOM kwa kushirikiana na wadau linatumia Sanaa za uchoraji mitaani ili kuelimisha jamii kuhusu jinsi ya kujikinga na ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19.

Michoro hiyo katika miji ya Agadez, Arlit na mji mkuu Niamey, inafuatia warsha iliyoendeshwa na IOM kwa ushirikiano na shirika la Sanaa ya mitaani bila mipaka, SASF mwaka 2019 ambapo watu zaidi ya 1,000 kutoka Niger peke yake walishiriki.

Takwimu za shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO, zinaonesha kuwa hadi sasa Niger ina wagonjwa 1.099 waliothibitishwa kuwa na COVID-19, ambapo kati yao hao 68 wamefariki dunia.

IOM inasema kuwa mwaka huu katikati ya janga la COVID-19, inaendelea na mpango huo katika nchi za Senegal, Ghana na Niger kwa lengo la kuimairisha uhusiano baina ya wahamiaji na jamii wenyeji huku wakichochea mjadala wa kupunguza kuenea kwa taarifa potofu na chuki dhidi ya wageni hasa wakati huu wa COVID-19.

Kwa usimamizi wa Eric, mchoraji nguli kutoka Niger,  wasanii wawili kutoka Togo wanaoishi Niamey na ambao walishiriki mafunzo ya mwaka jana, walipata fursa ya kuonesha kwa vitendo kile walichofundishwa mwaka jana ambapo walichora picha kwenye kuta za hospitali ya taifa mjini Niamey ikionesha wahudumu wa afya na nyingine kwenye barabara mashuhuri mjini humo.

Meya wa Arlit, Abdourahmane Dalahine anasema kuwa, “kusalamiana kwa mikono ni kitu ambacho kimeota mizizi katika utamaduni wetu. Hivi sasa tunabadili fikra hiyo katika mazingira haya magumu lakini tunaamini kuwa hakuna kinachoshindikana. Mpango huu umeleta hamasa sana kwenye jamii yet una tunatumai huu ni mwanzo.”

Kauli ya meya huyo wa Arlit inatokana na kwamba katika mchoro kwenye shule ya vijana, wanaonekana watu wakisalimiana kwa kugonganisha viwiko vya mikono yao.

Halikadhalika kwenye kuta nyingine, mchoro uliokuwa unasomeka, idumu baa sasa msanii amechena na maneno na kubandika mchoro wa mtu aliyevaa barakoa na kuandika, Naipenda Barakoa! Au “Bavette, j’adore!” kwa lugha ya kifaransa.

Kwa sasa mchoro huo umeenea katika maeneo mbalimbali ikiwemo makazi duni, baa, mijini na vitu vya makazi ya muda vya wahamiaji.

Akizungumzia michoro hiyo katika kuelimisha watu kuhusu COVID-19, Mkuu wa shule ya Mai Manga Oumara mjini Agadez, Alkassoum Halilou anasema kuwa, “picha inazungumza maneno elfu moja. Hata kama huelewi maandishi, kuona picha na kuhusisha na kuongeza uelewa, naamini itakuwa inaeleweka zaidi.”

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud