Vita nchini Yemen vyawatesa wagonjwa wa figo: WHO

17 Septemba 2018

Kuendelea kwa vita nchini Yemen kumezidisha machungu kwa wagonjwa wa figo ambao hivi sasa wanalazimika kusafiri muda mrefu kusaka huduma za kuondoa maji yanayojaa mwilini kama njia ya kusafisha figo zao.

Miongoni mwa wagonjwa hao ni Gailan Mohammed, ambaye kutokana na na kushindwa kumudu gharama za usafiri analazimika kutumia saa mbili kutembea kwa mguu kuifikia hospitali ya Al-Jumhoori ya mjini Sana’a kwa ajili ya kusafisha figo.

Akinukuliwa katika makala iliyochapishwa kwenye wavuti wa shirika la afya ulimwenguni, WHO kanda ya mashariki na Mediteranea, Gailan anasema “sina nguvu za kutembea lakini inanilazimu kwenda hospitali kwa kuwa siwezi kuvumilia maumivu.”

Gailan mwenye miaka 28, alilazimika kuhama kutoka jimbo la Taiz hadi mji mkuu wa Yemen Sana’a baada ya kituo chao cha matibabu huko Taiz kufungwa kutokana na mgogoro unaoendelea.

“Nilipohamia Sana’a kwa ajili ya matibabu niliishi katika banda la gari eneo la Faj Attan moja ya maeneo yaliyoathirika sana na vita. Siwezi kumudu kuishi popote” anaongeza Gailan.

OCHA/Charlotte Cans
Waliojeruhiwa na shambulizi la anga wakiwa katika hospitali ya Joumhouri, Sana'a, Yemen

Ingawa mwaka jana shirika la afya Duniani WHO lilisambaza vifaa ambavyo vingesaidia usafishaji wa figo kwa wagonjwa elfu 15 mjini Sana’a na jimboni Hudaydah na pia mwaka huu wakasambaza vingine elfu 60 katika miezi miwili iliyopita kwenye vituo vya kusafishia vipatavyo 32 nchini kote kwa ajili  ya  wagonjwa zaidi ya 5000, bado kuendelea kwa mgogoro nchini Yemen kumefanya uhitaji kuendelea kuwa mkubwa na kuwafanya wagonjwa wanaohitaji huduma ya kusafishwa figo kuwa hatarini.

Kabla ya mgogoro pamoja na kuumwa Gailan alikuwa anafanya kazi lakini alipoteza kazi yake kwasababu alihitaji muda kwa ajili ya kwenda kusafisha figo mara mbili kwa wiki.

Gailan anasema ni bahati nzuri kwamba matibabu yenyewe si ya kulipia vinginevyo angekuwa amepoteza maisha siku nyingi.

Kama ilivyo kwa Gailan, inakadiriwa kuwa wagonjwa 5200 ambao figo zao zimeshindwa kufanya kazi wako hatarini kupoteza maisha kutokana na uhaba wa vifaa vya kutolea maji katika figo ambavyo haviwezi kutosha kutoa huduma za kusafisha figo mara laki 7 kama inavyotakiwa kwa mwaka.

Abdulrahman Al Qudaimi akiwa anashindwa kuwatunza watoto wake tisa na wazazi wake wazee kijijini kwake, anaeleza alivyolazimika kuhama kutoka kijijini Haraz hadi Sana’a baada ya kugundulika kuwa ana tatizo la figo takribani miaka miwili iliyopita akiiacha nyuma familia yake yote.

“Sina yeyote hapa wa kuniangalia, ninaumwa sana na siwezi hata kutembea kwasababu ya maumivu miguuni mwangu. Lakini ninawezaje kumudu kumleta kijana wangu mmoja hapa kunisaidia wakati mimi mwenyewe ninaishi na ndugu kwasabbu siwezi kumudu gharama za kukodi mahali pangu mwenyewe?” anasema akigugumia kwa maumivu.

Wakati huu ambao mgogoro unaendelea kuvuruga hali ya afya, vituo vinne kati ya 32 vya kusafisha figo vimefungwa na vilivyobaki vikiwa na uhaba mkubwa wa vifaa na wagonjwa wengi.

 

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter