Nishati ya jua kuepusha milipuko ya kipindupindu Yemen

11 Julai 2018

Shirika la uhamiaji la Umoja wa Mataifa, IOM, limekabidhi kwa serikali ya Yemen mradi mkubwa wa maji unaotumisha nishati ya jua au sola ambapo miongoni mwa wafadhili ni Marekani na Ujerumani.

Mradi huo ulianza kupampu lita milioni moja za maji kila siku kwa wakazi 55,000 wa Shu'aub, Al Madinah Al Syahya na Sho'ob  wanaokabiliwa na uhaba wa maji.

Makabidhiano yamefanyika kwenye mji mkuu Sana’a ambapo paneli za sola 940 zimesimikwa katika shule tatu zilizopo kwenye majimbo ya Amanat Al Asimah na Sana'a.

Mkuu wa kitengo cha dharura nchini Yemen, Stefano Pes amesema mradi huo wa kuzalisha maji kwa kutumia nishati ya jua ni muhimu hasa kwa nchi hiyo ambayo asilimia 90 ya wakazi wake hawana huduma ya maji safi na salama.

Kwa mantiki hiyo amesema mradi huo utawezesha wakazi wa maeneo yaliyogubikwa na mzozo kuwa na njia mbadala ya kupata maji safi na salama.

Bwana Pes amesema watu wengi wanalazimika kutumia maji yasiyo safi na salama ambayo ni sababu kuu ya mlipuko wa hivi karibuni wa ugonjwa wa kipindupindu nchini Yemen.

Kupitia mradi huo wa kuzalisha maji kwa kutumia nishati ya jua au sola, takribani lita 150,000 za dizeli zitaokolewa huku tani 500 za hewa ya ukaa zitaepukwa kupitia mradi huo unaotumia nishati rafiki kwa mazingira.

Miongoni mwa wafadhili wa mradi huo ni Marekani na Ujerumani ambapo IOM inalenga kusambaza nchini kote Yemen ili hatimaye liwe taifa linalotumia nishati ya jua.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud