Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Biashara haramu ya wanyamapori inaweka hatarini afya na mazingira:UNODC

Tembo yatima aliyeokolewa huko David Sheldrick kituo cha  Wanyamapori Trust nchini Kenya.
UNEP/Natalia Mroz
Tembo yatima aliyeokolewa huko David Sheldrick kituo cha Wanyamapori Trust nchini Kenya.

Biashara haramu ya wanyamapori inaweka hatarini afya na mazingira:UNODC

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Janga la corona au COVID-19  linadhihirisha jinsi gani biashara haramu ya wanyamapori inavyotishia sio tu mazingira bali afya ya binadamu kwa mujibu wa ripoti mpya iliyotolewa leo na ofisi ya Umoja wa Mataifa ya madawa na uhalifu UNODC.

Ripoti hiyo “Uhalifu wa Wanyama pori duniani 2020” inaonyesha jinsi usafirishaji haramu wa baadhi ya wanyama pori ambao wanachinjwa na kuuzwa kiharamu unaweza kuongeza maambukizi ya magonjwa ambayo yanasambaa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu.

Magonjwa hayo kwa mujibu wa ripoti yanawasilisha asilimia 75 ya magonjwa yote ya mlipuko yanayoambukiza ikiwemo virusi vipya vya corona ambazyo sasa vimekuwa janga kubwa la kimataifa.

Katika ripoti hiyo mkurugenzi mtendaji wa UNODC Ghada Waly amesema “Mitandao ya uhalifu wa kimataifa wa kupangwa inajipatia faida kutokana na biashara haramu ya wanayama pori, lakini watu masikini ndio wanaolipa gharama ya uhalifu huo.”

Kakakuona ndio wanaosafirisha zaidi kiharamu

Ripoti hiyo imeelezea usafirishaji haramu wa baadhi ya wanyama kama kakakuona ambao umebainika kama unauwezekano mkubwa wa kuwa chanzo cha virusi vya corona. Hivi sasa wataalam wa shirika la afya duniani WHO wako njiani kuelekea nchini china katika juhudi za kubaini wanayama ambao ni chanzo cha COVID-19.

Ripoti inasema kati ya mwaka 2014 na 2018 kulikuwa na ongezeko kubwa la mara 10 la ukamatwaji wa magamba ya kakakuona yaliyokuwa yakisafirishwa kiharamu na hivyo kufanya wanayama hao kuwa ndio wanayama pori wanaosafirishwa zaidi kiharamu duniani.

Pia imesema karibu aina 6,000 za viumbe vilikamatwa katika muongo uliopita vikisafirishwa kiharamu wakiwemo wanyama, lakini pia mijusi, matumbawe, ndege na samaki.

Ripoti hata hivyo haikutaja nchi yoyote kuwa ndio chanzo cha zaidi ya asilimia 9 ya idadi yote ya wanayana na mimea iliyokamatwa ikisafirishwa kiharamu, huku washukiwa wa usafirishaji huo haramu wakiwasilisha takribani watu kutoka mataifa 150 na hivyo kudhihirisha kwamba asili ya uhalifu huu ni duniani kote.

Usafirishaji haramu wa mbao waongezeka

Ripoti hiyo pia imebainisha na kutathimini masoko ya usafirishaji haramu wa mbao, pembe za ndovu, pembe za vifaru, magamba ya kakakuona, jamii ya mijusi, paka shume na aina ya samaki kutoka Ulaya wanaofanana na nyoka.

Ripoti inasema mwenendo unaonyesha kwamba mahitaji ya pembe za ndovu na za vifaru kutoka Afrika yanapungua ikimaanisha kwamba masoko ya bidhaa hizo ni madogo kuliko ilivyopendekezwa hapo awali.  

Ripoti inakadiria kwamba bidhaa hizi mbili zilitengeneza zaidi ya dola milioni 600 kila mwaka kati ya mwaka 2016 na 2018.

Wakati huohuo mahitaji ya bidhaa za mbao yameongezeka kwa kiasi kikubwa katika miongo miwili iliyopita.

Na biashara haramu ya mbao kutoka Afrika imeingia kwenye mnyororo halali kwa ajili ya biashara ya samani. 

Pia ukamatwaji wa bidhaa za chui umeongezeka lakini wasafirishaji haramu wanania ya bidhaa za aina nyingine yap aka wakubwa ili watumike kama mbadala wa chui.

Mbali ya aina iliyozoeleka ya biashara sasa biashara hiyo imeingia katika njia ya kidijitali, na wasafirishaji haramu wamekuwa wakiuza mtandaoni  na kupitia apu mbalimbali wanyama walio hai na jamii ya mijusi kama nyoka na pia mifupa ya chui miongoni mwa vitu vingine.