Janga la COVID-19 limesababisha ongezeko la vifaa tiba bandia duniani:UNODC

8 Julai 2020

Ongezeko la ghafla la mahitaji ya dawa na vifaa tiba vya kukabiliana na janga la virusi vya corona au COVID-19 limesababisha ongezeko la usafirishaji haramu wa dawa na vifaa visivyo na viwango vinavyostahili au bandia kwa mujibu wa ripoti ya utafiti iliyochapishwa na ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na madawa na uhalifu UNODC. 

Ripoti hiyo iliyotolewa na UNODC hii leo mjiini Vienna Austria inasema “janga la COVID-19 limedhihirisha mapungufu yaliyopo katika mfumo wa sheria na ufuatiliaji wenye lengo la kuzuia utengenezaji na usafirishaji haramu wa bidhaa hizo ambazo ni tishio kubwa kwa afya ya umma.”

Akizungumzia changamoto hiyo mkurugenzi mtendaji wa UNODC Ghada Waly amesema “Afya na maisha ya watu yako hatarini wakati wahalifu wakitumia fursa ya janga la COVID-19 kujineemesha kwa fedha kutokana na hamasa ya watu na mahitaji ya vifaa vya kujikinga au PPE. Makundi ya kimataifa ya uhalifu wa kupangwa yanatumia mwanya uliopo katika mifumo ya ufuatiliaji ya kitaifa kuingiza dawa na vifaa badindia visivyokidhi viwango.”

Ameongeza kuwa “tunahitaji kuzisaidia nchi kuongeza ushirikiano ili kuziba mapengo, kuvijengea uwezo vyombo vya usalama na mfumo wa haki na sheria na kuelimisha umma kuhakikisha watu wako salama.”

Utafiti unaendelea katika kusaka chanjo na tiba ya virusi vya Corona, COVID-19
UN Photo/Loey Felipe
Utafiti unaendelea katika kusaka chanjo na tiba ya virusi vya Corona, COVID-19

Ripoti hiyo imesema magenge ya uhalifu wa kupangwa yameitumia hali ya sintofahamu inayozingira janga la COVID-19 kwa kuziba pengo la mahitaji ya madawa na vifaa tiba ambavyo ni haba na hivyo kusambaza vilivyo na viwango dunia au bandia.

Vifaa tiba bandia vina athari kubwa na mbaya kwa afya ya umma kwa kuwa huenda visitibu ipasavyo maradhi na vinaweza kuchangia hali ya dawa kuwa sugu mwilini imeongeza ripoti.

Ushahidi uliopo

Ushahidi wa ripoti unaonyesha kuwa matukio haramu kama vile udanganyifu, utapeli na kukusanya vitu vinavyohusiana na uzalishaji na usafirishaji haramu wa bidhaa zisizo na viwango vinavyostahili au bandia umeongezeka kufuatia kusambaa kwa virusi vya corona.

Ikitoa mfano ripoti imesema mathalani katika kisa kimoja hivi karibuni mamlaka ya afya ya Ujerumani  ilitoa tenda kwa kampuni mbili nchini Uswisi na Ujerumani kupitia kwenye mtandao wa makampuni hayo ili kutengeneza barakoa zenye thamani ya euro milioni 15  na baadaye ikabainika kwamba kumbe mtandao si wao lakini ni wa kampuni halali  na inayojulikana ya  nchini Hispania na kampuni hizo zimeutumia kiharamu kujipatia kipato.

Pia ripoti imesema wakati huu wa COVID-19 kumeshuhudiwa takwimu za uongo na uhalifu ikiwemo kutumia barua pepe bandia, kurubuni watu na biashara bandia wahalifu wakitumia wavuti za makampuni yanayofahamika na kushawishi wanunuzi kuwa wato ni makampuni halali.

Mabadiliko katika uhalifu wa kupangwa

Ripoti hiyo ya UNODC pia inatabiri kwamba tabia ya magenge ya uhalifu wa kupangwa itabadilika taratibu katika kipindi cha janga hili hususan wakati ambapo chanjo itapatikana  na magenge hayo huenda yakabadili mwelekeo kutoka kusafirisha kiharamu PPE na kuingia katika kusafirisha chanjo.

Mashambulizi ya mtandaoni dhidi ya miundombinu muhimu ya kushughulikia janga hili huenda yakaendelea katika mfumo wa utapeli mtandaoni ukilenga mamlaka za afya.

Hivyo ripoti inapendekeza kuwa kuimarisha mifumo ya sheria na faini na kuwa na mtazamo wa kimataifa wa kuharamisha utengenezaji na usafirishaji haramu wa vifaa tiba dunia au bandia ni muhimu kwani ni mtazamo wa Pamoja pekee ndio utawezesha kukabiliana na uhalifu huo unaoathiri watu na afya ya umma.

Lakini pia watu wanaofanya kwenye sekta ya afya watahitaji ujuzi mpya wa ziada kuweza kukabiliana na utapeli na uhalifu huo.

Mifano halisi ya vifaa tiba bandia

Mbali ya Ujerumani ripoti imetaja pia maeneo mengine ambako magenge ya kimataifa ya uhalifu wa kupangwa yametumia mwanya uliopo kutapeli, kufanya udanganyifu na kujineemesha kwa vifaa tiba bandia ikiwemo Uingereza ambako kituo cha kitaifa cha usalama wa mtandao NCSC,  kimesema kimefanikiwa kufunga biashara za kitapeli zaidi ya 2,000 zinazohusiana na virusi vya corona mwezi Machi mwaka huu na utapeli huo ulijumuisha maduka bandia yanayouza bidhaa za corona mtandaoni.

Nchini Ufaransa kwa mujibu wa ripoti serikali iliziondia mtandaoni wavuzi 70 za kitapeli zinazodai kuuza dawa aina ya Chloroquine mwezi Aprili mwaka huu.

Utapeli unaohusiana na COVID-19 uliofanyika Marekani ripoti imeutaja kuwa ni wa gharama ya dola milioni 13.4 tangu mwezi Januari hadi katikati ya Aprili 2020 na umewaathiri raia zaidi ya 18,000.

Katika miezi minne ya kwanza ya janga la COVID-19 kwa upande wan chi za Falme za Kiarabu au Emarati mashambulio 1,541 ya mtandaaoni yanyohusiana na COVID-19 yalibainika ikiwemo ya kutumia tishio la virusi vya malware, mashambulizi 621 ya kutumia barua pepe bandia na mashambulizi 145 ya kutumi auani au link bandia mtandaoni imesema ripoti.

Kwa vifaa tiba kama vipima joto au thermometer ambazo hazikidhi viwango na nyingine bandia Zaidi ya 3,000 zimekamatwa Thailand baada ya kusafirishwa kiharamu kupitia nchi zingine tatu na vipimajoto hivyo mbavyo havina ubora unaokubalika Ulaya pia vilikamatwa Italia.

Ripoti hiyo ya UNODC imesema magene ya uhalifu wa kupangwa kwenye eneo la Balkan Magharibi yanaaminika kujihusisha na biashara haramu ya utakatishaji fedha na kuwekeza katika kuzalisha na kusafirisha vifaa tiba bandia.

Na pia kumekuwepo kwa ripoti kuwepo na mashine za kusaidia kupumua ambazo hazikidhi viwango au za bandia nchini Urusi ambako uchunguzi dhidi ya utapeli huo umeanzishwa ikiwa ni Pamoja na Uingereza ambako baadhi ya mashine walizopokea hakukidhi viwango na zinauwezekano wa kusababisha hatari.Mashini hizo zisizo na ubora unaotakiwa zimeripotiwa pia Bosnia na Herzegovina kwa mujibu wa ripoti hiyo.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter