Wahalifu wanasaka kufaidika na COVID-19, tushirikiane kupambana nao:UNODC 

Uchunguzi wa polisi katika nchi zilizoendelea ni muhimu katika kukabiliana na uhalifu wa kimataifa wa kupangwa
UN Photo/Martine Perret
Uchunguzi wa polisi katika nchi zilizoendelea ni muhimu katika kukabiliana na uhalifu wa kimataifa wa kupangwa

Wahalifu wanasaka kufaidika na COVID-19, tushirikiane kupambana nao:UNODC 

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Wakati mitandao ya uhalifu kote duniani ikijaribu kusaka mbinu za kunufaika na janga la corona au COVID-19, ni muhimu kwa serikali kushirikiana na kufanyakazi pamoja kwa mujibu wa mktaba wa Umoja wa Mataifa wa kupambana na usafirishaji haramu wa binadamu, usafirishaji wa silaha na uhalifu miongoni mwa nchi , amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres. 

Kauli hiyo ameitoa leo kupitia ujumbe wa video kwenye mkutano wan chi zilizotia Saini mkataba wa Umoja wa Mataifa wa kupinga uhalifu wa kupangwa kwa kimataifa. 

Mwaka huu mkataba huo ambao hujulikana pia kama mkataba wa Palermo unatimiza miaka 20 tangu kupitishwa na mkuu wa Umoja wa Mataifa amesisitiza umuhimu wake hasa kwa wakati huu. 

COVID-19 kichocheo cha uhalifu 

Guterres amesema “Wahalifu wanasaka kufaidika na mgogoro wa COVID-19. Jasnga hili pia limedhihirisha hatari ya wahamiaji katika masuala ya usafirishaji kinyemela na haramu wa binadamu. Hivyo ushirikianio wa kimataifa kupitia mkataba wa kupinga uhalifu wa kupangwa wa kimataifa sasa unahitajika haraka kuluko wakati mwingine wowote.” 

Mkutano huo wa 10 wa nchi walizotia Saini mkataba huo, unaofanyika kwa juma zima umeandaliwa na ofisi ya Umoja wa Mataifa ya madawa na uhalifu UNODC

Dawa bandia na utapeli mtandaoni 

Katika hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano huo mkurugenzi mtendaji wa UNODC, Ghada Wally pia amesisitiza jinsi gani janga la COVID-19 linavyochochea shughuli za kihalifu. 

“Moja ya tishio kubwa linaloibuka hivi sasa na kuleta ahatari kwa Maisha ya binadamu ni uuzaji wa bidhaa za dawa bandia mtandaoni.Makundi ya uhalifu wa kupangwa yanauza bidhaa zisizokidhi viwango na bandia , yakiwalenga watu binafsi, vituo vya afya na mashirika ya umma kupitia utapeli wa mtandaoni. Chanjo batili za COVID-19 punde zitakuwa hali halisi yenye hatari kubwa hivyo serikali zinahitaji kujiandaa kupambana na tishio hili.” 

Hatua na kujikwamua na hatari hii 

Bi. Wally ameongeza kuwa mifumo ya huduma za afya inaendelea kukabiliwa na mashambulizi mtandaoni huku hatua za watu kusalia majumbani zimechochea ongezeko la ukatili wa kingono kwa Watoto mtandaoni. 

Wakati huohuo vikwazo vya kutotembea au kusafiri vimewafanya wahamiaji kuwa katika hatari zaidi ya kunyanyaswa na kusafirishwa kiharamu. 

Zaidi ya hapo amesema operesheni za uhalifu zinatishia hatua za kukabiliana na COVID-19 na kutia dosari katika mikakati ya kujikwamua na janga hilo. 

Makundi ya kihalifu amesema yamekuwa yakiiba fedha za msaada kutoka kwa wale wanaozihitaji zaidi na kupenyeza uchumi halali kupitia biashara haramu ya utakatishaji fedha. 

Kibarua muhimu kilichopo 

Nchi 190 ndio wanachama wa mkataba wa umoja wa Mataifa kupinga uhalifu wa kimataifa wa kupangwa ambao ndio mkataba pekee wa kimataifa unaobana kisheria dhidi ya tishio hili. 

Mkataba huo ulipitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwezi Novemba 2000 na kuanza kutekelezwa rasmi miaka mitatu baadaye. 

Mkataba huo ukatiwa nguvu zaidi na mikataba mingine midogo mitatu ya kupinga usafirishaji , usafirishaji kinyemela wa wahamiaji, utengenezaji wa bidhaa bandia na usafirishaji haramu wa silaha. 

Kazi kubwa iko mbele yetu juma hili wakati tukiadhimisha miaka 20 ya mkataba huu kwa kusongesha vita dhidi ya uhalifu wa kimataifa wa kupangwa , kuimarisha hatua za kuzuia na kuboresha ulinzi kwa waathirika wa uhalifu.” Amesema Bi. Wally. 

Na kuongeza kuwa “Tumekusanyika sote hapa ana kwa ana na kupitia mtandao kwa sababu tunaamini katika nguvu ya mkataba na vipengele vyake katika kusaka suluhu za matatizo ambayo hakuna nchi inayoweza kuyakabili peke yake, na kuhakikisha jamii zetu ziko salama na zinaweza kuchanua.”