Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mradi wa UNHCR Mauritania wasaidia kuleta nuru kwa wakimbizi kutoka Mali

Ukanda wa Afrika Mashariki unahitaji kupatia vijana wake stadi sahihi ili kuweza kuziba pengo la ajira.
UN/Eritrea
Ukanda wa Afrika Mashariki unahitaji kupatia vijana wake stadi sahihi ili kuweza kuziba pengo la ajira.

Mradi wa UNHCR Mauritania wasaidia kuleta nuru kwa wakimbizi kutoka Mali

Wahamiaji na Wakimbizi

Nchini Mauritania, mradi wa mafunzo ulioendeshwa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR na wadau wake, umesaidia wakimbizi kutoka Mali kuweza kupata stadi za kujipatia kipato kutunza familia zao na kujiandaa vyema kurejea nyumbani pindi hali itakapokuwa shwari.

 

Miongoni mwa wanufaika wa mradi huo ni Farka , mkulima kutoka Niafunke nchini Mali, ambaye ni baba watoto 12 kutoka kwa wake zake wawili.

Farka alikimbia Mali akiwa na familia yake mwaka 2012 kufuatia mapigano yaliyoanzishwa na waasi na kuishia kwenye kambi ya wakimbizi ya Mbera mpakani mwa Mali na Mauritania.

Katika makazi  yao mapya ya Hodh Ecchargui nchini Mauritania, Farka na wakimbizi wengine 60,000 kutoka Mali wamekuwa wakiishi kwa kutegemea msaada kutoka UNHCR lakini kutokana na msaada huo kutoweza kukidhi mahitaij yao yote, UNHCR na wadau ilianzisha mradi.

Mradi huo ulijumuisha Farka na watu wengine 15 na uliwapatia stadi za kutengeneza nyaya za kuzungushia ua.

Halikadhalika UNHCR na wadau wake hao ambao ni shirika la kazi la Umoja wa Mataifa, ILO, Muungano wa Ulaya, EU ,Marekani na Japan wameanzisha Chuo cha Mafunzo ya Ujenzi kwenye kambi ya Mbera ikiwapatia mafunzo na ajira wakimbizi na jamii za wenyeji, wake kwa waume.

Kutokana na mafunzo hayo, wanufaika wamejenga shule na hivi sasa wako katika harakati za ujenzi wa barabara.

Halikadhalika UNHCR inasema vijana 200 wamepata stadi za ufundi bomba, ufundi uashi na hata uzalishaji wa nishati endelevu na stadi za masoko.

Pamoja na kuchangia katika uchumi wa jamii inayowahifadhi, wakimbizi hao wako tayari kurejea nyumbani wakiwa na stadi na hivyo kuwa mashuhuda wa utekelezaji wa mkataba wa kimataifa wa wakimbizi wa kuhakikisha wanakuwa na fursa sawa ukimbizini kama wenyeji.