Skip to main content

Mauritania yapatia vyeti vya kuzaliwa wakimbizi wa Mali

Watoto wakimbizi kutoka Mali waliozaliwa kambi ya Mbera nchini Mauritania wakipatiwa hati ya cheti cha kuzaliwa.
UNHCR
Watoto wakimbizi kutoka Mali waliozaliwa kambi ya Mbera nchini Mauritania wakipatiwa hati ya cheti cha kuzaliwa.

Mauritania yapatia vyeti vya kuzaliwa wakimbizi wa Mali

Wahamiaji na Wakimbizi

Heko Mauritania kwa kuanza kuwapatia vyeti vya kuzaliwa watoto ambao ni wakimbizi kutoka Mali walioko nchini  humo.

Ni pongezi kutoka shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR kufuatia wakimbizi hao walioko kambi ya MBera kusini-mashariki mwa Mauritania kuanza kupatiwa nyaraka hizo.

Msemaji wa UNHCR huko Geneva, Uswisi, Cécile Pouilly amesema watoto hao 7600 ni wale waliozaliwa kambini humo.

Hatua hiyo kwa mujibu wa Bi. Pouilly itasaidia kuondoa madhila mengi kwa watoto ikiwemo kuwaepusha na ndoa katika umri mdogo, jambo ambalo ni tatizo kubwa kwenye kambi hiyo.

Mwaka 2017 pekee, UNHCR ilipata visa 97 kambini Mbera vya ndoa za watoto ikihofia kuwa pengine idadi inaweza kuwa kubwa zaidi.

Kazi ya utoaji vyeti vya kuzaliwa kwa watoto ilizinduliwa katikati ya mwezi huu kwa watoto waliozaliwa kwenye kambi hiyo na mfumo umewekwa ili wengine wote watakaozaliwa nao wapatiwe nyaraka hiyo.

Ghasia za tangu mwaka 2012 kaskazini mwa Mali zimesababisha maelfu ya raia kukimbilia nchi jirani ikiwemo Niger, Burkina Faso na Mauritania.