Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Idara ya zimamoto mjini Juba Sudan Kusini yaishukuru UNMISS kwa msaada wake wa magari

Mlinzi wa kikosi cha kulinda amani Sudan Kusini kutoka China akiwa anashika doria mjini Juba.Picha
UNMISS(Picha ya Maktaba July 2018)
Mlinzi wa kikosi cha kulinda amani Sudan Kusini kutoka China akiwa anashika doria mjini Juba.Picha

Idara ya zimamoto mjini Juba Sudan Kusini yaishukuru UNMISS kwa msaada wake wa magari

Amani na Usalama

Mamlaka mjini Juba Sudan Kusini zimeushukuru Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS ambao umetoa msaada wa magari mawili makubwa ya huduma za uzimaji moto katika nchi hiyo ambayo miundombinu yake na huduma za kijamii vimeharibiwa na vita ya wenyewe kwa wenyewe iliyodumu kwa takribani miaka mitano.

Kutokana na uwepo wa gari moja pekee la zima moto ambalo hata hivyo mara kwa mara limekuwa likiharibika, imekuwa haiwezekani kwa mamlaka kutoa msaada unaohitaji katika mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba. Hilo limekuwa ni tatizo kwani mara nyingi moto umekuwa ukiharibu masoko, makazi ya watu na hata kusababisha vifo hususani katika mji huo mkuu ambako jamii inaishi na kufanya kazi katika hali za msongamano.

Sasa magari haya mawili makubwa yatasaidia sana kwani yatatumiwa na wataalamu wenyeji wa uzimaji moto ambao mara zote wamekuwa wakitegemea usaidizi kutoka kwa maafisa wa UNIMISS pindi moto unapotokea. Kwa muda mrefu hiyo imekuwa changamoto kwani UNMISS yenyewe ina wafanyakazi wanne tu wa kimataifa wa kuzima moto ambao kwa kushirikiana na wataalamu wenyeji, wamekuwa wakilazimika kudhibiti moto kila unapotokea, saa 24, siku 7 za wiki. Mkuu wa UNMISS, David Shearer anasema,

 “Ninafahamu kuwa mna magari machache ya kuzima moto kwas asa na tumekuwa tukikusaidieni katika siku za nyuma, lakini ninatumai magari haya mawili, moja lina injini ambayo inasukuma takribani lita 250 kwa dakika moja na jingine ni tenki ambalo linabeba lita 10,000 za maji, ambayo ina maanisha mnaweza kwenda mahali na kuna moto, kutakuwa na maji ya kutosha kuuzima moto.”

Pamoja na magari, UNMISS pia imetoa vifaa vya kujikinga zikiwemo suruali na jaketi, buti pamoja na kofia ngumu na vifaa vingine. Mkrugenzi wa huduma ya uzimaji moto katika jimbo la Equatoria ya kati, Meja Jenerali Pascal Lado anashukuru,

“Umewakuwa wakati mzuri wa kuwa na askari wa zima moto wa UNMISS kwasababu wakati wowote kulipokuwa na moto mjini Juba, tungeweza kuomba msaada kwa UNMISS na majibu yao yalikuwa ya haraka. Sasa kwa kuwa wametupatia malori, tutaweka juhudi zetu ili kulinda maisha ya watu na mali ili waweze kuishi kwa raha.”

Wataalamu wa UNMISS wanatoa maelekezo ya jinsi ya kuyatumia magari haya kwa wenzao wa Sudan Kusini. Wakati askari wa zima moto wa Sudan Kusini wakiondoka katika eneo la makabidhiano kwa furaha wakiyaendesha magari yao haya mapya, UNMISS imeahidi kutoa mafunzo zaidi na msaada kuhakikisha kwa pamoja wanaweza kuwalinda raia na mali zao ili waweze kuuona mstakabali mpya ulio bora.